Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mahojiano

Capoeira ya Brazil yaleta ahueni kwa watoto waliotumikishwa DRC

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, mzozo Mashariki mwa nchi hiyo umetumbukiza watoto na vijana katika kutumikishwa vitani. Hata hivyo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF linahaha kila uchao kuwanasua watoto hao kutoka mikono ya watumikishaji.

Baada ya kuwanasua, UNICEF huwaweka vijana katika kambi ya mpito ili kuwapatia stadi za maisha na waweze kutengamana na jamii na miongoni mwao ni ile iliyoko Goma ambako vijana huishi kwa muda wa wiki tano. Je hufanya nini? Kwa undani ungana na Assumpta Massoi kwenye Makala hii.

Madhila wanayokumabana nayo watu wenye ulemavu katika kampeni dhidi ya Ebola

Watu wenye ulemavu wanoishi katika jamii zisizo na mazingira mujarabu kwa  kundi hilo, hukumbana na madhila kadhaa. Watu hao wenye ulemavu hupata wakati mgumu zaidi pale kunapokuwa na hali za dharura mathalani ugonjwa wa homa kali ya Ebola.Ugonjwa huu ambao ulizitikisa nchi za Afrika Magharibi ikiwamo Sierra Leone unatajwa kutokomea kwa sasa kutokana na idadi ndogo ya visa. Lakini ni kwa namna gani watu wenye uleamvu wanahusishwa katika kampeni dhidi ya Ebola? Ungana na Joseph Msami katika makala ifuatayo.

Narudi nyumbani nikiwa askari bora zaidi- Ngondi

Meja Jenerali Leonard Ngondi amemaliza muda wake kama mkuu wa vikosi vya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Liberia UNMIL.

Katika mahojiano na idhaa hii, amesema kwamba amejifunza mengi na anarejea nyumbani Kenya akiwa askari bora kuliko alivyokuwa wakati alipochukua nafasi hiyo takriban miaka miwili iliyopita.

Baada ya kuwasilisha ripoti yake hapa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, Meja Jenerali Ngondi  amezungumza na Grace Kaneiya, na hapa anaanza kwa kutaja mafanikio yake makubwa wakati akishikilia nafasi ya mkuu wa vikosi vya UNMIL.

Profesa Ali Mazrui aenziwa UM

Miezi minne baada ya kuaga dunia jijini New York, Marekani, Hayati Profesa Ali Mazrui msomi na nguli wa fasihi kutoka Kenya amefanyiwa hafla maalum kwenye Umoja wa Mataifa jijini New York kutokana na mchango wake kwenye shughuli za Umoja huo. Mathalani ushiriki wake kwenye mradi wa uandishi wa historia ya Afrika unaotekelezwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi, Elimu na UTamaduni, UNESCO ambapo yeye alihariri juzuu ya Nane ya mradi huo.

Vita dhidi ya Ebola vyakwamisha jamii kijijini Sierra Leone

Baada ya visa 25 vya Ebola kuibuka kwenye kijiji cha Aberdeen, nchini Sierra Leone, kijiji kizima kimewekwa kwenye karantini.

Watalaam wa afya wa serikali ya Sierra Leone, mashirika yasiyo ya kiserikali na wafanyakazi wa kijamii wanafuatilia waliokua karibu na magonjwa ili kukomesha mlipuko kwenye eneo hilo.

Lakini, wakati huo huo, shughuli zote za uchumi zimekwama, mathalani wavuvi hawawezi tena kwenda kuvua samaki. Kulikoni? Ungana na Priscilla Lecomte kwenye makala hii.

Sintofahamu mashariki mwa Ukraine na madhila kwa wananchi.

Nchini Ukraine, mapigano yanayoendelea mashariki mwa nchi hiyo yameacha wananchi wengi katika dimbwi la sintofahamu, wakihaha kutwa kucha kusaka hifadhi. Mathalani familia zimekosa cha kufanya, shughuli za kujipatia kipato zimeyoyoma huku amani nayo ikiwa imesalia kuwa ni ndoto licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa hivi karibuni. Je hali halisi ikoje? Ungana na Joseph Msami kwenye makala hii.

Ushirikiano wa kimataifa wahitajika ili kutunza bayonuai baharini: UNEP

Hifadhi ya bayoanuai iliyopo baharini ni changamoto kubwa hasa wakati ambapo asilimia 64 ya maeneo ya bahari hayamilikiwi na nchi yoyote. Kwa mujibu wa Dixon Waruinge, mtalaam wa Shirika la Umoja wa Mataila la Mpango wa Mazingira, UNEP, ni muhimu mashirika ya kimataifa yaungane ili kubaini mbinu za kudhibiti maeneo haya.

Katika mahojiano na Priscilla Lecomte, Waruinge amezingatia pia hifadhi ya bayoanuai iliyopo kwenye maeneo yaliyo ndani ya mipaka ya nchi za ukanda wa Afrika ya Mashariki.

Lugha ya mama na mustakhbali wake

Tarehe 21 mwezi Februari kila mwaka ni siku ya lugha ya mama duniani! Lengo ni kuhamasisha matumizi ya lugha ya mama katika  nyanja mbali mbali ikiwemo kielimu. Kila msichana na mvulana, mwanamke na mwanamume ni lazima awe na nyenzo muhimu kama vile lugha ili aweze kushiriki katika maswala muhimu katika jamii popote alipo.Licha ya umuhimu wa lugha ya mama, baadhi ziko hatarini kutoweka.Kauli mbiu mwaka huu ni  elimu jumuishi kupitia lugha; Lugha ina umuhimu!

Redio ni chombo adhimu kwa jamii kaskazini mashariki mwa Kenya

Umuhimu wa redio katika jamii mbalimbali ni dhahiri ikizingatiwa kwamba chombo hiki kinatumika kwa mawasiliano na maswala mbalimbali ya kijamii. Pia redio ni daraja ya mawasiliano kati ya wananchi na serikali, hususan katika maeneo ya pembezoni. Nchini Kenya baadhi ya jamii za pembezoni zimekuwa zikitengwa lakini sasa uwepo wa radio umefungua mlango wa mawasiliano. Basi ungana na Geoffrey Onditi wa redio washirika KBC, katika makala hii.