Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Habari kwa Ujumla

Hali ya mjane kutoka Uganda ni msumari wa moto juu ya kidonda-sehemu 2

Wakati Umoja wa Mataifa ukichagiza nchi kuhakikisha kwamba hakuna mtu anayeachwa nyuma kuelekea ukomo wa malengo ya maendelo endelevu yaani SDGs bado kuna changamoto ambazo huenda zikakwamisha ufikiaji wa malengo hayo. Wanawake na waisichana mara kwa mara wanakabiliwa na aina mbali mbali ya ubaguzi ikiwemo suala la urithi wa mali hususan katika jamii zilizoko nchi zinazoendelea.

Keating ajadilia amani na usalama na wanawake viongozi Somalia

Mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na mkuu wa mpango wa Umoja huo nchini Somalia UNSOM Michael Keating, leo amekuwa mwenyeji wa mkutano wa wanawake viongozi wa Somalia kuzungumzia azimio nambari 1325 la baraza la usalama kuhusu wanawake, amani na usalama.

Amessisitiza kwamba mchango wao na wanawake wengine katika jamii ni muhimu hasa katika kuleta amani, kuzuia na kutatua migogoro, kujadili amani, na kuzuia na kulinda wanawake na wasichana dhidi ya vita.

Hewa chafuzi kutoka kwenye kilimo itaendelea kwa mwiba kwa tabianchi- FAO

Shirika la chakula na kilimo, FAO limesema kiwango cha hewa chafuzi kutoka katika shughuli za kilimo kitaongezeka siku zijazo na kuleta madhara katika tabianchi.

Mkurugenzi Mkuu wa FAO José Graziano da Silva amesema hayo leo huko Bonn, Ujerumani kwenye mkutano wa 23 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, COP23.

Kwa mantiki hiyo amesisitiza umuhimu wa kuzingatia mbinu bora za kilimo, usafiri na ulaji wa chakula akisema bila kufanya hivyo maisha ya mamilioni ya watu yako hatarini.

Guterres akutana na Aung San Suu Kyi huko Manila

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliyeko ziarani barani Asia amekuwa na mazungumzo na kiongozi mkuu wa Myanmar, Daw Aung San Suu Kyi.

Mazungumzo hayo yamefanyika huko Manila, Ufilipino, kando mwa kikao cha viongozi wa umoja wa nchi za kusini na mashariki mwa Asia, ASEAN.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa amesema viongozi hao wawili wamejadili hali katika jimbo la Rakhine wakati huu ambapo mamia ya maelfu ya warohingya wa madhehebu ya kiislamu wanakimbilia Bangladesh kutokana na mateso.

Guterres asisitiza umuhimu wa ushirikiano katika kongamano la ASEAN

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António  Guterres amesema utandawazi unatoa fursa mpya lakini wakati huo huo unaongeza tofauti ya usawa wa kiuchumi na kijamii, kuongeza wasiwasi na kuweka shinikizo kwa ushirikiano wa kijamii.

Bwana Guterres akizungumza huko Manila Ufilipino katika kongamano la umoja wa nchi za Kusini-Mashariki mwa Asia, ASEAN amesema mabadiliko ya tabianchi yanachangia visa vya vimbunga na dhoruba huku akipongeza viongozi wa ASEA kwa hatu za kukabiliana na hatari za mabadiliko ya tabianchi na majanga ya asili.

Viua vijasumu ni hazima tutumie kwa uangalifu- WHO

Wiki ya kuhamasisha umma kuhusu usugu wa viua vijasumu imeanza leo ambapo shirika la  afya ulimwenguni WHO linataka jamii ifahamu umuhimu wa kupunguza matumizi ya dawa hizo kwa wanyama na binadamu kama njia mojawapo ya kuepusha matumizi yasiyo sahihi na yasiyo ya lazima.

Kupitia wavuti wake, WHO inasema usugu husababisha dawa hizo kushindwa kufanya kazi yake pindi mnyama au binadamu anapokumbwa na maradhi na hivyo kusababisha kifo.

Kwa hali hiyo WHO inasema tiba za kawaida zinashindikana na kusababisha magonjwa kuenea kwa wanyama na binadamu.

Wahamiaji 25 walioko Libya wahamishiwa Niger wakisubiri makazi ya kudumu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limehamisha wahamiaji 25 kutoka Libya kwenda Niger baada ya kubainika kuwa wanaishi kwenye mazingira magumu na hatari zaidi.

Msemaji wa UNHCR huko Geneva, Uswisi Cécile Pouilly amesema miongoni mwao ni wanawake 15 na watoto wanne ambapo sasa wanasubiri maombi yao ya kuhamishiwa nchi ya tatu yaweze kukamilika.

Bi. Poilly amesema wahamiaji hao wanatoka Eritrea, Ethiopia na Sudan ambapo wawakilishi kutoka nchi ambazo zinataka kuwachukua ndio wanaendelea na tathmini ili kupatiwa makazi mapya.

Picha: UM/Idhaa ya Kiswahili

Ibara kwa Ibara- Tamko la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa

Tamko la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa mwezi disemba mwaka 2018 linatimiza miaka 70. Tamko hilo ni msingi wa haki za binadamu ulimwenguni na lilipitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 1948. Kwa kutambua umuhimu wake, ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa inaanza kampeni ya kulipigia chepuo. Nasi kwenye Idhaa ya Kiswahili tunakuletea ibara za tamko hilo. Ibara ziko 30 nasi tunakuletea ibara moja kila siku. Hii leo tunakuletea Ibara ya kwanza na Selina Jerobon.

Ibara ya 3: Kila mtu ako na haki ya kuishi, haki ya kuwa huru na kulindwa

ILO

ILO yapendekeza sera kutokomeza ajira kwa watoto ifikapo 2025

Ripoti ya shirika la kazi duniani  ILO imesema kuimarisha ulinzi wa kisheria, usimamizi wa soko la ajira, ulinzi wa kijamii na upatikanaji wa elimu bora na mazungumzo baina ya jamii, serikali na wadau ni muhimu katika kukabiliana na tatizo la ajira kwa watoto.

Ripoti hiyo kwa jina, kumaliza ajira kwa watoto ifikapo 2025: Tathmini ya sera na program,  imetolewa leo wakati ambapo wadau wamekusanyika Buenos Aires katika kongamano la kimataifa kuhusu kutokomeza ajira kwa watoto.