Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ILO yapendekeza sera kutokomeza ajira kwa watoto ifikapo 2025

ILO yapendekeza sera kutokomeza ajira kwa watoto ifikapo 2025

Pakua

Ripoti ya shirika la kazi duniani  ILO imesema kuimarisha ulinzi wa kisheria, usimamizi wa soko la ajira, ulinzi wa kijamii na upatikanaji wa elimu bora na mazungumzo baina ya jamii, serikali na wadau ni muhimu katika kukabiliana na tatizo la ajira kwa watoto.

Ripoti hiyo kwa jina, kumaliza ajira kwa watoto ifikapo 2025: Tathmini ya sera na program,  imetolewa leo wakati ambapo wadau wamekusanyika Buenos Aires katika kongamano la kimataifa kuhusu kutokomeza ajira kwa watoto.

ILO inasema sera pekee haziwezi kutokomeza ajira kwa watoto na utokomezaji hautowezekana bila sera muafaka kwani licha ya kwamba asilimia 99.9 ya watoto walio kati ya umri wa miaka 5-17 wanalindwa na mkataba wa ILO wa 1999 ambao umetiwa saini na nchi 181 lakini kuweka vigezo hivi kuwa sheria ya kitaifa bado ni changamoto.

Kwa mujibu wa makadirio ya kimataifa yaliyochapishwa Septemba mwaka 2017 watoto milioni 152 walio na umri wa kati ya miaka 5-17 sawa na mtoto mmoja kati ya kumi wanatumikishwa katika ajira kwa watoto duniani.

Ajira kwa watoto imepungua tangu 2000 lakini mwenendo ulipunguza kasi tu kati ya mwaka 2012 na 2016 na kwa muktadha huo, watoto milioni 121 watakuwa bado katika ajira za utotoni ifikapo mwaka 2025.

Photo Credit
ILO