Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahamiaji 25 walioko Libya wahamishiwa Niger wakisubiri makazi ya kudumu

Wahamiaji 25 walioko Libya wahamishiwa Niger wakisubiri makazi ya kudumu

Pakua

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limehamisha wahamiaji 25 kutoka Libya kwenda Niger baada ya kubainika kuwa wanaishi kwenye mazingira magumu na hatari zaidi.

Msemaji wa UNHCR huko Geneva, Uswisi Cécile Pouilly amesema miongoni mwao ni wanawake 15 na watoto wanne ambapo sasa wanasubiri maombi yao ya kuhamishiwa nchi ya tatu yaweze kukamilika.

Bi. Poilly amesema wahamiaji hao wanatoka Eritrea, Ethiopia na Sudan ambapo wawakilishi kutoka nchi ambazo zinataka kuwachukua ndio wanaendelea na tathmini ili kupatiwa makazi mapya.

Amepongeza kitendo hicho cha nia njema kutoka Niger akisema hata hivyo mipango ya aina hiyo ni michache wakati huu ambapo jamii ya kimataifa itakosa mkakati sahihi wa uhamiaji halali huku watu wakikimbia machafuko au mizozo inaposhindwa kupatiwa suluhu.

(Sauti ya Poilly)

 “Tunatarajia kuhamisha wengine zaidi siku za usoni lakini hii itategemea ahadi za kupatia wahamiaji makazi mapya na iwapo zitakuwa zinatosheleza. Kamishna Mkuu wa UNHCR ametoa wito wa dharura miezi kadhaa iliyopita ya kutaka fursa zaidi elfu 40 za makazi katika njia za kuelekea Mediteranea ya Kati lakini hadi sasa wito huo umetekelezwa kidogo.”

Kwa mujibu wa shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM, mwaka huu pekee watu wapatao 3,000 wamefariki dunia wakijaribu kuvuka bahari ya Mediteranea kuelekea Ulaya.

Photo Credit
Wahamiaji katika kizuizini nchini Libya. Picha: Shirika la Uhamiaji wa Umoja wa Mataifa (IOM) / 2017