Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres asisitiza umuhimu wa ushirikiano katika kongamano la ASEAN

Guterres asisitiza umuhimu wa ushirikiano katika kongamano la ASEAN

Pakua

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António  Guterres amesema utandawazi unatoa fursa mpya lakini wakati huo huo unaongeza tofauti ya usawa wa kiuchumi na kijamii, kuongeza wasiwasi na kuweka shinikizo kwa ushirikiano wa kijamii.

Bwana Guterres akizungumza huko Manila Ufilipino katika kongamano la umoja wa nchi za Kusini-Mashariki mwa Asia, ASEAN amesema mabadiliko ya tabianchi yanachangia visa vya vimbunga na dhoruba huku akipongeza viongozi wa ASEA kwa hatu za kukabiliana na hatari za mabadiliko ya tabianchi na majanga ya asili.

Guterres amerejelea wasiwasi wake kuhusu tishio la ugaidi kimataifa ikiwemo katika eneo hilo na kukumbusha utayari wa Umoja wa Mataifa kusaidia wanachama wa ASEAN katika juhudi za kukabiliana na ugaidi, uuzaji wa mihadarati na usafirishaji haramu wa binadamu kwa kuweka sera ambazo zitalinda raia na sheria zinazo heshimu haki za binadamu.

Akisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kukabiliana na baadhi ya changamoto hizo amesema

(Sauti ya Guterres)

“ASEAN na wanachama wake wamefanya jitihada katika kumaliza mizozo kwa miongo mitano iliyopita. Mmeonyesha dhamira yenu kwa amani ya kimataifa na usalama kupitia ushiriki wenu kwenye operesheni za amani za Umoja wa Mataifa.”

Ameongeza kuwa hawezi kuficha wasiwasi wake juu ya mamia ya maelfu ya wakimbizi kutoka Myanmar wanaoelekea Bangladesh na wakati huo huo kukaribisha juhudi za ASEAN katika kutoa msaada wa kibinadamu jimbo la Rakhine Kaskazini.

Guterres ametaja maendeleo endelevu na jumuishi kama njia sahihi katika kuzuia mizozo na ugaidi na ni kiini cha ajenda ya 2030 na pia katika malengo ya jamii ya ASEAN ya 2025.

Ametolea wito nchi za ASEAN kuongeza maradufu dhamira yao kuimarisha ushrikiano wa nchi hizo na Umoja wa Mataifa.

Photo Credit
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres anakaribishwa na Rais wa Ufilipino Rodrigo Duterte na First Lady Bi. Honeylet Avancena katika mtano wa Mataifa ASEAN. Picha: UNIC / Maria Teresa Debuque