Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Habari kwa Ujumla

UN Photo/Turkey

Bunge lamwondoa madarakani Rais wa Brazil

Kufuatia kitendo cha bunge la Brazil kupiga kura kuridhia kushtakiwa kwa rais wa nchi hiyo, Dilma Rousseff, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema ametambua hatua hiyo sambamba na ile ya kuapishwa kaimu rais Michel Temer kushika madaraka hayo.

Taarifa ya msemaji wake imemnukuu akimtakia kila la heri Rais Temer anapoanza awamu hiyo ya uongozi akisema ana imani na Brazil chini ya uongozi wake na kwamba Umoja wa Mataifa utaendelea na udau wa karibu na nchi hiyo.

Wanawake Darfur wajifunza kiingereza

Moja ya mamlaka iliyopewa Ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika huko Darfur,Sudan(UNAMID) katika kuongoza shughuli zake za kulinda amani ni kuchangia katika mazingira salama kwa ajili ya ujenzi wa uchumi na maendeleo. Elimu ni kina cha maendeleo na walinda amani polisi wanawake wa UNAMID wamelitambua hilo, na katika makala hii tutasikia mchango wao kwa wanawake katika kambi ya wakimbizi wa ndani.

Kampeni kubwa ya chanjo dhidi ya polio kufanyika Afghanistan

Nchini Afghanistan, kampeni kubwa ya chanjo dhidi ya polio imeanza leo kwa watoto wote wenye umri wa chini ya miaka mitano, kwa kuwa ugonjwa huo hulipuka kati ya mwezi Septemba na Oktoba.

Shirika la afya duniani, WHO limesema kampeni hiyo inayofanywa kwa ushirikiano baina yake, wizara ya afya ya umma nchini humo na shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF inatekelezwa na wafanyakazi wa afya wapatao 65,000.

Wahudumu hao wenye mafunzo watakwenda hadi maeneo ya kuvuka mpaka na Pakistani ambako kuna wakimbizi zaidi ya milioni moja na nusu wa Afghanistani.

Jeshi la Syria na ISIS walitumia silaha za kemikali- Ripoti

Uchunguzi uliofanyika kwa ridhio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa umebaini kuwepo kwa matukio matatu ya matumizi ya silaha za kemikali nchini Syria tangu mwezi Aprili mwaka 2014.

Uchunguzi huo huru na usiogemea upande wowote uliendeshwa na jopo la watu watatu kupitia mfumo wa uchunguzi wa pamoja, JIM ambapo waliangazia visa tisa vya matumizi ya silaha za kemikali na hivyo walipaswa kubainisha ni nani walitumia.

Virginia Gamba ni mkuu wa JIM na akihojiwa na Cristina Silveiro wa Radio ya Umoja wa Mataifa amesema..

(Sauti ya Virginia)

De Mistura ahuzunishwa na kuendelea kwa mapigano Syria

Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Syria, Staffan de Mistura amesema anasikitishwa mno na kuendelea kwa mapigano na hali ya hatari ya kibinadamu nchini humo.

Katika taarifa yake, amesema mchakato wa kisiasa na suluhu la kisiasa ndio njia pekee ya kumaliza mgogoro huo na hali ilivyo kwa sasa.

Ameongezea kuwa majadiliano kati ya Urusi na Marekani wiki hii ni muhimu kwa jitihada za kurejesha ukomeshaji wa uhasama.

Heko Myanmar kwa hatua za maridhiano- Ban

Akiendelea na ziara yake huko barani Asia, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amekutana na kiongozi mshauri wa Myanmar Aung San Suu Kyi ambapo amesema wamejadili masuala kadhaa ikiwemo zahma inayokumba watu wa jamii ya Rohingya katika jimbo la Rakhine.

Katika mkutano na wanahabari uliofanyika mji mkuu Naypyidaw na kumjumuisha pia Bi. Aung, Ban amesema wamekubaliana kuwa wananchi wa Myanmar bila kujali kabila, dini au hali ya kiuchumi, wanahitaji fursa bora za kijamii na kiuchumi kwenye mazingira ambamo kwayo kila mmoja anakuwa huru, sawa na salama.

Vyama vya ushirika vyakomboa wakimbizi nchini Uganda

Uganda, nchi ambayo inahifadhi idadi kubwa ya wakimbizi wengi wao kutoka Sudan Kusini inapongezwa katika juhudi zake za kubadili maisha ya wakimbizi kwa kuwapa uwezo wa kujimudu na kuboresha maisha yao kwa mfano kumiliki ardhi na kupata vibali vya kufanya biashara.

Katika makala hii ya John Kibego tutasikia jinsi vyama vya ushirika vinavyowasaidia wakimbizi hususan wakulima kujikwamua kiuchumi.

Mradi wa kuboresha takwimu za sekta za nje waanzishwa na Shirika la Fedha Duniani

Shirika la fedha duniani, IMF, hii leo limezindua mradi wa miaka mitatu wa kuboresha takwimu za sekta katika nchi za Afrika ya Kati na a Magharibi.

Mradi huo umeanzishwa katika taasisi ya mafunzo ya Afrika, ATI, huko nchini Mauritius na umewezeshwa kwa msaada mkubwa wa serikali ya Japan.

Mradi huo una lengo la kuimarisha takwimu za sekta za nje, kuleta ubora na kufunga mapengo katika maeneo muhimu kama vile urari wa malipo, nafasi ya kimataifa ya uwekezaji na takwimu za nje za madeni.

Vifaa vya matibabu vyawasili Taiz, Yemen

Shirika la afya duniani WHO na msaada wa kituo cha misaada ya kibinadamu cha mfalme Salman limetoa msaada wa tani kumi na mbili za vifaa vya matibabu ya dharura kwa jiji la Taiz nchini Yemen.

Taarifa ya WHO imesema vifaa hivyo ni pamoja na dawa za kutibu kipindupindu na vifaa vya kusaidia watoto wanaozaliwa, unatarajiwa kusambazwa kwa wakazi wa jiji hilo pamoja na hospitali za Al- Thawra, Al-Modhaffar na Al- Ta'aon ambako wamekumbwa na ghasia za kivita

Israel sitisha mipango ya ujenzi Yerusalem mashariki- Mladenov

Mratibu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu mchakato wa amani mashariki ya kati, Nickolay Mladenov ameitaka Israel kuachana na mipango yake ya ujenzi wa makazi mapya kwenye eneo inalokalia la Palestina.

Amesema hayo wakati akiwasilisha ripoti yake kwa njia ya video kwa wajumbe wa Baraza la Usalama waliokutana leo kujadili hali ya mashariki ya kati hususan suala la Palestina.

Mladenov amesema tangu mwezi Julai Israeli imekuwa ikisongesha mipango ya kujenga nyumba 1,000 huko Yerusalem Mashariki na makazi mengine Ukingo wa Magharibi wa mto Jordan.