Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Habari kwa Ujumla

Wakwepa kodi wanalindwa, wafichua taarifa wanashtakiwa- Mtaalamu

Wafichua taarifa ni mashujaa wa zama za sasa na wanatekeleza majukumu yao kwa maslahi ya jamii na haki za binadamu hivyo hawapaswi kushtakiwa kwa kutoa taarifa kuhusu ukwepaji kodi. #luxleaks

Hiyo ni kauli ya mtaalam huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu uendelezaji wa utaratibu wa kimataifa wa demokrasia na haki, Alfred de Zayas aliyotoa kufuatia ripoti za kuhukumiwa kwa waliotoa taarifa kuhusu sakata la Lux.

Umoja wa Mataifa wateua atakayetetea haki za wapenzi wa jinsia moja

Baraza la Haki za Binadamu, leo limeamua kumteua mtaalam maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu ukatili na ubaguzi dhidi ya wapenzi wa jinsia moja na watu wanaojitambua kwa jinsia tofauti na maumbile (LGBT).

Uamuzi huo umefikiwa baada ya mjadala uliohitimishwa baada ya rasimu ya azimio la kufanya uteuzi huo kufanyiwa marekebisho mara 11, likiungwa mkono na nchi wanachama 23, huku wanachama 18 wakilipinga. Wanachama sita hawakuonyesha kuegemea upande wowote.

Ni hatua kubwa kufikisha misaada kulikozingirwa:Egeland

Kufikishwa kwa msaada katika maeneo mawili ya mwisho yaliyozingirwa Syria, ambayo hajakuwa na msaada wowote kutoka nje tangu 2012 kunadhihirisha hatua kubwa kabisa ya kibinadamu umesema Alhamisi Umoja wa Mataifa.

Ujumbe huo ni kutoka kwa Jan Egeland, mratibu wa kikosi kazi cha kimataifa cha masuala ya kibinadamu kwenye Umoja wa Mataifa mjini Geneva baada ya misaada ya kibinadamu kuwasili maeneo ya Arbin na Zamalka vijijini Damascus.

Ban akaribisha uamuzi wa China kujiunga na IOM

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amekaribisha Uchina kujiunga na shirika la kimataifa la uhamiaji IOM.

Ban amesema anaamini kwamba China itakuwa mchango mkubwa na muhimu kwa IOM.

Uchina kuwa mwanachama wa IOM ni muhimu hasa katika wakati huu ambapo masuala ya wahamiaji na wakimbizi yanahitaji kushughulikiwa na hatua kuchukuliwa haraka kuliko wakati mwingine wowote.

Marekani imetangaza msaada wa dola milioni $52 zaidi kwa wakimbizi wa Palestina

Ufadhili wa ziada kwa wakimbizi wa Palestina wa jumla ya dola milioni 51.6 umetangazwa na serikali ya Marekani Alhamisi ili kukidhi ombi la msaada wa dharura lililotolewa.

Shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Palestina UNRWA lilitoa ombi la msaada wa dharura ili kusaidia kazi zake katika maeneo ya Wapalestina yanayokaliwa.

Msaada huu umekuja kipindi muhimu na muafaka kabisa wakati mahitaji ya dharura yakiongezeka amesema afisa wa UNRWA Sandra Mitchell.

Baraza la haki za binadamu lakaribisha maridhiano Sri Lanka kwa tahadhari

Maridhiano nchini Sri Lanka baada ya miongo ya vita vya wenye kwa wenyewe yanafanyika sasa , lakini bado kuna kazi kubwa ya kufanya ili kuwafikisha kwenye mkono wa sheria waliokiuka haki za binadamu , amesema leo kanishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa mataifa Zeid Ra’ad Al Hussein.

Akizungumza kwenye baraza la haki za binadamu mjini Geneva, Bwana Zeid amekaribisha mabadiliko ya serikali kuhusu masuala yanayojumuisha udhibiti mkubwa katika jeshi.

Ufadhili wa kibinadamu unapungua, misaada zaidi yahitajika kwa watu Fallujah- UM

Umoja wa Mataifa umeeleza kutiwa wasiwasi na mzozo wa kibinadamu unaoibuka huko Fallujah, nchini Iraq, ambapo watu zaidi ya 20,000 wamekuwa wakikimbia makwao tangu tarehe 22 Mei.

Katika ziara yake, Mratibu wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya kibinadamu nchini Iraq, Lise Grande, amekutana na watu walioweza kukimbia na kufikia maeneo salama huko Ameriyat al Fallujah, mashariki mwa mkoa wa Anbar.

Bi Grande amesema walizungumza na familia za watu walioweka maisha yao hatarini na kuukimbia mji wa Fallujah, wakihadithia matukio ya kuvunja moyo.

UN Photo/Ari Gaitanis

Ban ateua kikosi-kazi cha mizozo ya kiafya duniani

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ametangaza leo wanachama wa kikosi kazi chake kuhusu mizozo ya kiafya duniani.

Kikosi-kazi hicho kiliundwa na Katibu Mkuu kwa minajili ya kusaidia na kufuatilia utekelezaji wa mapendekezo yaliyofanywa na jopo la ngazi ya juu kuhusu jitihada za kimataifa panapoibuka mizozo ya kiafya.

Suluhu ya kuwa na mataifa mawili, Israel na Palestina inawezekana

Amani baina ya watu wa Israel na Palestina inawezekana na kila liwezekanalo lifanywe kuhakikisha hilo, amesema Jumatano Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon.

Ujumbe huo ni kwa ajili ya wote wanaoshiriki mkutano kwenye Umoja wa Mataifa Geneva, ambao unatathimini ni jinsi gani ya kusukuma mbele mchakato wa amani baina ya Israel na Palestina.

Mtazamo wowote wa muafaka wa baadaye ni kuundwa kwa taifa la Palestina kwenye maeneo yanayokaliwa na Israel tangu vita vya Mashariki ya Kati vya mwaka 1976, kwa kile kinachoitwa suluhu ya mataifa mawili.

Sina uhakika bado na tarehe ya mazungumzo Syria- de Misturra

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na kikao kuhusu hali ya Mashariki ya Kati likijikita zaidi suala la Syria ambapo limepokea taarifa ya kila mwezi ya mjumbe maalum wa Katibu Mkuu kuhusu nchi hiyo, Staffan de Misturra.

Kikao hicho kilikuwa cha faragha ambapo baada ya kumalizika de Misturra amezungumza na waandishi wa habari mjini New York, Marekani na kueleza kuwa shambulio la kigaidi huko Istanbul, Uturuki ni kumbusho kwa wajumbe wa baraza kuwa vita dhidi ya ugaidi ni jambo linalohitaji mwendelezo.