Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Habari kwa Ujumla

Viongozi wa Afrika waongee na sauti moja kuhusu mabadiliko ya Umoja wa Mataifa: Ban

Mkutano wa 26 wa Muungano wa Afrika ukiendelea mjini Addis Ababa Ethiopia, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameeleza kwamba uwakilishi katika Baraza la Usalama ni moja ya kipaumbele cha Umoja wa Mataifa, lakini ni wajibu wa nchi wanachama kuelewana kuhusu mabadiliko wanayotaka kutekeleza.

Bwana Ban amesema hayo leo akizungumza na waandishi wa habari mjini Addis Ababa, ambapo aliulizwa kuhusu jinsi ya kuimarisha uwakilishi wa Afrika katika mfumo wa Umoja wa Mataifa na hasa Baraza la Usalama, ambalo ni suala lililoibuka katika mkutano wa Muungano wa Afrika.

Ban ki-moon azungumzia mzozo wa Burundi na viongozi wa Rwanda na Burundi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amemwambia Naibu Rais wa Burundi Joseph Butore kwamba mchakato wa kisiasa unapaswa kuwa jumuishi, endelevu, na kuungwa mkono na jumuiya ya kikanda na kimataifa ili kupata suluhu kwa mzozo unaoendelea nchini humo.

Bwana Ban amesema hayo akizungumza na Bwana Butore leo kuhusu hali ya kiusalama, haki za binadamu na kibinadamu nchini Burundi, kando ya mkutano wa Muungano wa Afrika ulioanza leo mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Bwana Ban ameisihi serikali ya Burundi kuendelea kuwa na uwazi kuhusu hali iliyo nchini humo.

Ban Ki-moon ampongeza Rais Kenyatta kwa juhudi zake Somalia

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amezungumzia hali ya usalama nchini Somalia na rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, akishukuru mchango wa Kenya katika ujenzi wa amani nchini Somalia, na kusisitiza umuhimu wa kuwa na mkakati thabiti wa kupambana na mizizi ya itikadi kali na katili.

Mazungumzo hayo yamefanyika leo kando ya mkutano wa 26 wa Muungano wa Afrika mjini Addis Ababa Ethiopia.

Ban Ki-moon apongeza viongozi wa Afrika wanaoacha madaraka kwa kuheshimu katiba

Akizungumza leo kwenye ufunguzi wa kikao cha 26 cha Muungano wa Afrika, mjini Addis Ababa, Ethiopia, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amewaomba viongozi wa Afrika wafuate mfano wa viongozi wanaocha madaraka kwa kuheshimu katiba za nchi zao.

Ameongeza kwamba uchaguzi ni mtihani kwa utawala bora, huku nchi 17 za Afrika zikitarajia kufanya uchaguzi mwaka huu.

(Sauti ya bwana Ban)

Mkataba wa Paris kutoka COP21 umeanza kuzaa matunda:Pasztor

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya mabadiliko ya tabianchi ambaye amemaliza muda wake, Janos Pazstor, amesema mkataba wa mabadiliko ya tabianchi uliopitishwa mwaka jana Paris, Ufaransa umeanza kuzaa matunda.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani, Bwana Pasztor amesema dhihirisho hilo limetokana na ahadi zilizoanza kutekelezwa hata na sekta binafsi hususan katika nishati jadidifu au nishati mbadala.