Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afya na usalama wa watoto wakimbizi wa Rohingya 500,000 njia panda:UNICEF

Msichana mdogo anabeba mtoto mgonjwa kwenye Kituo cha Matibabu cha Jeshi katika Kambi ya Wakimbizi ya Kutupalong, Makazi ya muda. Picha: OCHA / Anthony Burke

Afya na usalama wa watoto wakimbizi wa Rohingya 500,000 njia panda:UNICEF

Usalama na afya ya watoto wakimbizi wa Rohingya zaidi ya nusu milioni wanaoishi katika kambi zilizo na msongamano mkubwa na makazi yasiyo rasmi nchini Bangladesh iko hatarini limeonya leo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF. Tupate taarifa Zaidi na Selina Jerobon

(TAARIFA YA SELINA JEROBON)

Onyo hilo la UNICEF limekuja wakati msimu wa vimbunga na mvua za Monsoon ukijongea nchini Bangladesh , likisema kwamba hali ya kibinadamu ambayo tayari ni mbaya kwa watoto zaidi ya 520,000 sasa huenda ikawa zahma kubwa.

Maelfu ya watoto watakabiliwa na hatari ya magonjwa, mafuriko, maporomoko ya udongo na pia watoto kutawanywa zaidi.

Kwa mujibu wa Edouard Beigbeder mwakilishi wa UNICEF Bangladesh maji yasiyo salama , upunguvu wa vifaa vya usafi na mazingira machafu vinaweza kusababisha mlipuko wa kipindupindu na homa ya ini aina ya E, magonjwa ambayo hukatili haraka maisha ya kina mama wajawazito na watoto. Christopher Boulierac ni msemaji wa UNICEF

(SAUTI YA CHRISTOPHER BOULIERAC)

Ameongeza kuwa msimu huo  wa monsoon pia utaweka hatarini makazi ya wakimbizi, mfumo mzima wa maji, vyoo na miundombinu mingine ambayo inasaidia wakimbizi wa Rohingya zaidi ya 650,000 walioingia Bangladesh tangu Agosti 2017.