Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Makubaliano ya utatu ndio muarobaini kwa warohingya kurejea Myanmar- UNHCR

UNHCR imewapatia Wakimbizi wa Rohingya vifaa muhimu kutoka kituo cha usambazaji katika kambi ya Kutupalong ili kuwawezesha kurejea makazi yao. Picha: © UNHCR / Hall ya Andy

Makubaliano ya utatu ndio muarobaini kwa warohingya kurejea Myanmar- UNHCR

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limesema limejiandaa kwa ajili ya majadiliano ya kuwezesha wakimbizi wa Rohingya kurejea nyumbani kufuatia makubaliano kati ya Myanmar na Bangladesh tarehe 23 mwezi uliopita.

UNHCR inasema ingawa haikuwa sehemu ya mpango huo tayari imejiandaa kujadili pia vigezo vya wakimbizi hao kurejea ambapo msemaji wa UNHCR huko Geneva, Uswisi, Adrian Edwards amewaambia waandishi wa habari kuwa..

(Sauti ya Adrian Edwards)

“UNHCR, haikuwa sehemu ya makubaliano lakini imetajwa kwenye nyaraka husika. Mipanog ya sasa ni kuanzisha kikundi kazi cha pamoja ndani ya wiki tatu tangu kutiwa saini kwa nyaraka hiyo. Tuko tayari kuwa sehemu ya kikosi hiki na kusaidia serikali hizo mbili kufanya kazi itakayowezesha wakimbizi kutekeleza haki  yao ya msingi ya kurejea nyumbani kwa uhuru, usalama na kwa utu. Kwa mtazamo wetu, jambo hili linapaswa kujumuisha makubaliano ya utatu.”

Bwana Edwards amerejelea msimamo wa shirika hilo kila mkimbizi ana haki ya msingi ya kurejea nyumbani lakini hilo linapaswa kufanyika kwa hiari na pale mtu anapohisi kuwa wakati na mazingira ya kufanya hivyo  yako sahihi.

Amesema wakimbizi watahitaji taarifa sahihi kuhusu hali ilivyo kwenye makazi yao ya awali huko Myanmar na kwamba uamuzi wao unapaswa kufanyika wakiwa na taarifa kamili.