Viongozi wa dunia waombwa kujitahidi kutokomeza ueneaji wa silaha za nyuklia

27 Aprili 2015

Kongamano la kutathmini Mkataba wa kuzuia ueneaji wa silaha za nyuklia (NPT) limeanza leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York ambapo nchi wanachama wa mkataba huo watajadili tathmini hiyo kwa kipindi cha mwezi mmoja.

Katika ujumbe alioutoa kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Naibu Katibu Mkuu Jan Eliasson amesema kutokomeza silaha za nyuklia kumewekwa kipaumbele cha juu na Umoja wa Mataifa.

Hivyo Bwana Eliasson amewasihi viongozi wa dunia kuongeza bidii ili kuimarisha mkataba huo ili kutokomeza ueneaji wa silaha za nyuklia.

Aidha amesikitishwa na mwelekeo wa miaka mitano iliyopita unaoonyesha kwamba baadhi ya nchi zimeongeza kutumia silaha hizo licha ya mafanikio yaliyopatikana kuanzia 1990 hadi 2010, akiongeza kwamba mwelekeo huo ni dalili ya kurejelea kwa fikra za vita baridi.

“ Nawaomba viongozi waachane na msimamo wa kisiasa unaoangalia muda mfupi mbele. Licha ya hayo, nawaomba kuwa na dira ya kimataifa itakayotimiza mahitaji ya jamii nzima. Usalama wa kitaifa wa ukweli hauwezi kufikiwa iwapo bado kutakuwepo na tishio la nyuklia. Tishio hilo linapaswa kusitishwa kwa ajili ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo”

Tathmini ya Mkataba wa kuzuia ueneaji wa silaha za nyuklia inafanyika kila miaka mitano tangu kuridhiwa kwa mkataba huo mwaka 1970.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter