Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kwa wakazi wengi wa vijiini Afrika huduma bora ya afya bado ni ndoto: ILO

Kwa wakazi wengi wa vijiini Afrika huduma bora ya afya bado ni ndoto: ILO

Ripoti mpya ya shirika la kazi duniani, ILO inaonyesha kuwa asilimia 56 ya watu wanaoishi vijiini hawana huduma za msingi za afya, idadi ambayo ni maradufu ya wale wa mijini wasiopata huduma kama hizo. Taarifa zaidi na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Ripoti hiyo iitwayo ushuhuda wa dunia kuhusu ukosefu wa uwiano wa huduma za afya kati ya mijini na vijijini imehusisha mataifa 174 ikiweka bayana kuwa bara la Afrika ndio linaongoza kwani asilimia 83 ya wakazi wake wa vijijini hawana huduma hizo.

ILO inatupia lawama uwekezaji mdogo kwenye sekta ya afya kwa miongo kadhaa licha ya kwamba afya ni haki ya msingi ya binadamu na inapaswa kupatiwa wakazi wote bila kujali maeneo wanayoishi.Kama hiyo haitoshi, hata pale kwenye miundombinu ya afya bado wahudumu wa afya nao ni tatizo.

Xenia Scheil-Adlung, mratibu wa sera za afya kutoka ILO akisema kuondoa tofauti serikali isitegemeze suala la afya kwenye misaada bali iwe haki kisheria na kwamba…

(Sauti ya Xenia)

“Ni muhimu kusambaza pia kwa uwiano sawa ufadhili muhimu katika maeneo ya vijijini kama ilivyo maeneo ya mjini na mara nyingi hiyo inahitaji ugatuzi wa mifumo ya afya .”

Kwa mujibu wa ripoti hiyo nchini Somalia, Guinea, Niger na Chad takribani asilimia 99.8 hawapati huduma za afya.