Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa 69 wa Baraza Kuu waanza rasmi: Kutesa ataka nchi zisikate tamaa

Rais wa Baraza Kuu la UM Sam Kutesa. (Picha:UM)

Mkutano wa 69 wa Baraza Kuu waanza rasmi: Kutesa ataka nchi zisikate tamaa

Mkutano wa 69 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa umeanza rasmi Jumanne ya tarehe 16 Septemba mjini New Yew York, Marekani ambapo Rais wa Baraza Sam Kutesa amesema nchi wanachama zina fursa ya kihistoria ya kuandaa ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015.

Akihutubia nchi wanachama katika kikao cha kwanza cha mkutano huo, Kutesa amesema mkutano unaanza wakati jumuiya ya kimataifa imegubikwa na msururu wa changamoto ambazo hazikutarajiwa, kuanzia umaskini, njaa, ukosefu wa ajira, ugaidi, mizozo ya kivita, mabadiliko ya tabianchi na jipya zaidi mlipuko wa Ebola.

Hata hivyo amesema;

“Ingawa mtazamo unaweza onekana wa kukatisha tamaa na changamoto ni nyingi, hatupaswi kugubikwa na hofu na kupoteza matumaini. Kwa pamoja, kwa kujituma na kwa mtazamo mmoja tunaweza kufikia mambo makubwa.”

Ilikufanikisha maudhui ya mkutano wa 69 aliyotangaza mara baada ya kuteuliwa ambayo ni Kufanikisha na kutekeleza ajenda ya mabadiliko baada ya mwaka 2015, Bwana Kutesa amesema ataitisha mikutano mitatu ya ngazi ya juu.

Mmoja utafanyika Februari ukiangazia utekelezaji wa ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015, wa pili mwezi Machi ukimulika usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake na wa tatu utafanyika mwezi Aprili kuhusu utatuzi wa migogoro kwa njia ya amani.

Halikadhalika amesema ataitisha mkutano kuhusu mabadiliko ya tabianchi mwezi Juni mwaka 2015.

Bwana Kutesa amegusia pia marekebisho ya Baraza la Usalama akitaka nchi wanachama kupitia msukumo sualahilokupitia majadiliano baina ya nchi.