Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ISIL inanufaika kutokana na kutoumaliza mzozo wa Syria

UN Photo - Jean-Marc Ferre
Paulo Pinheiro, Chairman of the Independent Commission of Inquiry on Syria.

ISIL inanufaika kutokana na kutoumaliza mzozo wa Syria

Jamii ya kimataifa kutochukua hatua kuumaliza mzozo wa Syria kumeendelea kuyapa moyo makundi yanayozozana kutenda ulaifu yakijua hayatowajibishwa, na hivyo kutia chachu katika mgogoro huo ambao umelikumba taifa hilo. Hayo yamesemwa na Kamisheni ya Kimataifa inayochunguza ukiukwaji wa haki za binadamu nchini humo.

Tume hiyo imesema walionufaika hivi karibuni na kulegea kwa jamii ya kimataifa ni kundi la wanamgambo wanaotaka kuanzisha dola la Kiislamu, ISIL.

Katika ripoti yake kwa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, tume hiyo imesema kuwa kuibuka kwa ISIL ni mbiu ya wito kwa serikali na makundi makuu ya upinzani kutafuta njia ya pamoja ya kulegeza misimamo yao mikali ili kufikia makubaliano ya kina kisiasa.

Ripoti hiyo inaweka dhahiri uhalifu uliotekelezwa na serikali ya Syria, ukiwemo kurusha mabomu kiholela katika maeneo yanayokaliwa na raia, utesaji, ukatili wa kingono, na kuizingira miji inayopinga serikali.

Inasema pia kuwa kundi la ISIL limetekeleza mauaji ya halaiki, na kuwaua wanawake, pamoja na kuwafanya watoto kushuhudia viwango vya juu vya ukatili, ukiwemo mauaji ya hadharani.

Paulo Sérgio Pinheiro ni mwenyekiti wa tume hiyo ya uchunguzi.

“ISIS na makundi ya upinzani yenye silaha sio pekee wanaotekeleza mauaji na uharibifu Syria. Serikali ya Syria bado ndiyo inayoongoza kusababisha vifo vingi zaidi vya raia kwa kuua na kulemaza makumi ya raia kila siku. Vituo vya upekuzi aghalabu huwa mwanzo tu wa safari hatairishi ya kutoweka, kuteswa, kubakwa na kwa wengi, kifo. Mzozo wa Syria hautasuluhishwa kwenye kitali cha vita. Njia pekee ya kuumaliza mzozo na ukatili ni mazungumzo baina ya serikali na makundi makuu ya upinzani, kwa uungwaji mkono wa mataifa yenye ushawishi na Umoja wa Mataifa.”

Kamisheni hiyo imesema kuwa mataifa yaliyokuwa yakijiandaa kuchukua hatua dhidi ya ISIS ni lazima yazingatie sheriaza vita, na kufanya kila juhudi kulinda uhai wa raia.