Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kujua kusoma na kuandika kunaweza kuleta maendelo endelevu

Shule ya Msingi ya Hoima mjini Hoima. Picha: John Kibego/Radio Spice FM

Kujua kusoma na kuandika kunaweza kuleta maendelo endelevu

Kujua kusoma na kuandika ni moja ya njia muhimu ya kuleta maendeleo endelevu, kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO.

Jumatatu Septemba Nane ikiwa ni siku ya kimataifa ya kujua kusoma na kuandika, Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO Irina Bokova amesema watu wanaojua kusoma na kuandika wanawezeshwa kuchukua uamuzi unaofaa katika mambo ya kiuchumi, ustawi wa jamii au mazingira, akiongeza kwamba wanawake wanaojifunza kusoma wanachangia katika kuleta maendeleo endelevu.

Aidha, UNESCO imesisitiza kwamba vita na mizozo vinachangia katika kuzuia watoto kwenda shuleni, takwimu zikionyesha kwamba asilimia 42 ya watoto wanaoishi kwenye nchi maskini zilizoathirika na mizozo hawaendi shuleni.

Halikadhalika wataalamu wa UNESCO wameongeza kwamba, wakina mama wote wakiwa wamepata elimu ya msingi, vifo vya watoto vingepungua kwa asilimia 15.