Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lamulika hatma ya watoto katika mizozo

Leila Zerrougui(kushoto) Mwakilishi wa Katibu Mkuu kuhusu watoto na mcheza filamu Forest Whitaker(kulia), Balozi Mwema wa UNESCO kuhusu Amani na Maridhiano

Baraza la Usalama lamulika hatma ya watoto katika mizozo

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, limefanya leo mjadala wa wazi ulioangazia ripoti ya Katibu Mkuu ya hivi karibuni kuhusu hatma ya watoto katika mizozo ya silaha. Taarifa kamili na Grace Kaneiya

(Taarifa ya Grace)

Mjadala wa leo katika Baraza la Usalama umeng’oa nanga kwa kumsikiliza Mwakilishi wa Katibu Mkuu kuhusu watoto katika maeneo ya mizozo, Leila Zerrougui, ambaye amesema ingawa hatua zimeendelea kupigwa katika kuwalinda watoto vyema zaidi, mizozo mipya inazima ufanisi huo.

“Baraza hili limefahamishwa kuhusu Syria mara kwa mara na hali huko bado ni mbaya kwa watoto. Karibuni mmezuru Sudan Kusini na Somalia na kujionea hali huko. Matukio yanayoibuka nchini Iraq yamechangia kuongezeka kwa ukiukwaji mkubwa unaofanywa na pande zote katika mzozo.”

Bi Zerrougui ameorodhesha maeneo mengine yenye mizozo na jinsi inavyoathiri watoto

“Migogoro na hali tete Libya, Afghanistan, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Mali na Sudan Kusini vinaendelea kutishia hali ya wanyonge, na wanahjitaji juhudi zetu zote kuwalinda.”

Mwingine aliyezungumza ni mcheza filamu Forest Whitaker, balozi mwema wa UNESCO kuhusu amani na maridhiano, ambaye pia ametoa uungaji mkono kwa kampeni ya “Watoto sio Wanajeshi”

“Nilipoanza kujishughulisha na watoto vitani miaka kumi iliyopita, na kusikia hadithi zao, nilitambua athari zitokanazo na kuishi katika mizozo kama mtoto. Kwa hiyo hii ni fursa kwangu mimi kusema kuwa haikubaliki kwa watoto kutumiwa katika ukatili kwa njia yoyote ile.”

Wengine waliozungumza kwenye kikao cha leo ni Bwana Hervé Ladsous, ambaye ni Mkuu wa Operesheni za Ulinzi wa Amani katika Umoja wa Mataifa, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Yoka Brandt.