Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban Ki-moon: Jamii ya kimataifa iwajibike kulinda raia duniani

Ban Ki-moon: Jamii ya kimataifa iwajibike kulinda raia duniani

Baraza Kuu la Umoja la Mataifa limekutana katika makao makuu mjini New York kujadili ripoti ya Katibu Mkuu inayotathmini jitihada zilizofanyika ili kulinda raia duniani. Taarifa zaidi na Priscilla Lecomte.

(Taarifa ya Priscilla)

Katika hotuba yake mbele ya baraza Kuu, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amesema, tangu kuundwa kwa mkakati wa Umoja huo unaotaka Umoja wa Mataifa kuwajibika kulinda raia, mafanikio yamepatikana lakini vile vile changamoto ni nyingi kutokana na mizozo inayotisha huko Iraq, Syria, Sudan Kusini na kadhalika.

Amesema raia wanateseka nchi wanachama zinaposhindwa kuwalinda, akifafanua..

“Kushindwa kukabiliana na mitazamo mikali inayosambaza chuki na inayotumia ubaguzi kwa lengo la kisiasa, kushindwa kwa nchi wanachama kulinda raia wake na kushindwa kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua mapema mbele za viashiria vya uhalifu na kuchukua hatua ipasavyo uhalifu ukishatokea.”

Amesisitiza kwamba, jamii ya kimataifa haiwezi tena kupuuzia uhalifu hizo, bali inapaswa kuwajibika kwa pamoja ili kuzuia uhalifu na kulinda raia.

Ripoti ya Katibu Mkuu inaonyesha jinsi gani nchi wanachama na jamii ya kimataifa zinaweza kupambana na mizizi ya mauaji ya kimbari, na uhalifu wa kibinadamu, Bwana Ban akizingatia umuhimu wa kuimarisha ngvu za serikali ili ziwe na uwezo wa kupambana na changamoto kadhaa kama vile vyama venye msimamo mkali.

Wajibu wa kulinda raia ni mkakati ulioamuliwa na Umoja wa Mataifa na viongozi wa nchi wanachama katika Kongamano la Dunia la 2005.