Wanawake na watoto wote wanastahili kupewa fursa sawa maishani: Ban
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon, ameliambia kongamano la ubia kuhusu afya ya waja wazito na watoto mjini Johannesburg kuwa ni lazima kuwepo usawa katika kuwasaidia wanawake na watoto ambao wanakabiliwa na hatari ya utaka na vifo.
Katika ujumbe alioutoa kwa njia ya video, Bwana Ban amesema kuwa katika kipindi cha miaka mine, mkakati wa Kila Mwanamke na Kila Mtoto umedhihirisha kuwa ubia unaokoa maisha, akiongeza kuwa sasa wanawake na watoto wachache zaidi wanafariki kutokana na sababu zinazoweza kuzuiwa au kutibiwa.
Hata hivyo, Ban amesema bado hatua zinapigwa kwa mwendo wa pole sana, akiongeza kuwa uwekezaji na ubia zaidi unahitajika ili kuepusha vifo vya watoto na waja wazito:
“Iwapo tutaongeza uwekezaji, kuangazia usawa na kuchagiza haki za binadamu, tunaweza kuwa na ulimwengu ambapo hakuna vifo vya waja wazito na watoto ambavyo vinaweza kuzuiliwa, katika kizazi kimoja tu. Ufanisi baada ya mwaka 2015 unatutegemea kufanya kazi pamoja na kubuni ubia imara ndani na nje ya sekta ya afya.”
Katibu Mkuu amesema, kwa pamoja, ndoto ya kuwepo ulimwengu ambapo kila mwanamke na kila mtoto anafikia uwezo wake inaweza kutimia.