Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

Mukhtasari wa mikutano katika Makao Makuu

Kwenye ukumbi wa Baraza la UM juu ya Uchumi na Jamii (ECOSOC), hii leo, panafanyika majadaliano ya kuzingatia mfumo unaofaa kudhibiti bora mizozo na kuimarisha operesheni za ulinzi amani kimataifa. Kikao hiki kimeandaliwa na Ofisi ya Raisi wa Baraza Kuu la UM pamoja Jumuiya ya Wabunge wa Kimataifa (IPU).

Hapa na Pale

Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP) limefufua tena huduma zake za kiutu katika jimbo la Somaliland, shughuli ambazo zililazimika kusitishwa kufuatia mashambulizi ya mabomu katika mji wa Hargeysa yaliotukia tarehe 29 Oktoba, na moja ya mabomu hayo yalilenga majengo ya ofisi ya Shirika la UM juu ya Miradi ya Maendeleo (UNDP). WFP iligawa tani 522 za chakula katika wiki iliopita, kwa kupitia miradi kadha iliopo nchini kwa sasa.~

Maelezo mafupi juu ya hali katika JKK

Hii leo asubuhi Baraza la Usalama limekutana kuzingatia azimio liliowakilishwa na Ufaransa kuhusu uwezekano wa kuongeza wanajeshi 3,000 ziada wa kimataifa, wanaohitajika kuimarisha ulinzi wa amani katika JKK, kufuatia mapigano yaliopamba kwenye eneo hili la Maziwa Makuu mnamo wiki za karibuni.~

BU linasailia maendeleo Usomali

Baraza la Usalama, leo asubuhi, vile vile limezingatia ripoti ya KM juu ya hali katika Usomali. Miongoni mwa masuala yaliojadiliwa ni pamoja na hali ya usalama nchini, haki za binadamu na athari za kiutu kwa umma wa Usomali kutokana na kupwelewa kwa utekelezaji wa mapatano ya Djiboouti yaliofikiwa baina ya Serikali ya Mpito na Umoja wa Makundi ya Ukombozi wa Pili wa Usomali.

UM unaadhimisha Siku Kuu ya Watoto Duniani

Tarehe 20 Novemba inaadhimishwa rasmi na UM kuwa ni Siku ya Watoto Duniani. Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) limekaribisha, kwa nguvu kubwa, uamuzi wa baadhi ya vijana walioshiriki, katika siku za nyuma, kwenye mapigano wangali na umri mdogo, wa kuanzisha mtandao mpya utakaotumiwa kuamsha hisia za umma wa kimataifa juu ya shida wapatazo watoto kwenye maeneo ya migogoro na mapigano.

Siku ya Kuhamasisha Maendeleo ya Viwandani Afrika

UM unaadhimisha Siku ya Kukuza Maendeleo ya Viwanda Afrika. Risala ya KM kuihishimu siku hii ilitilia mkazo ya kuwa shughuli za kukuza viwanda katika Afrika ikitekelezwa itaashiria hatua itakayosaidia pakubwa kudhibiti, kwa mafanikio, matatizo ya chakula, fedha na athari za mabadiliko ya hali ya hewa na, hatimaye, kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na jamii ili kuufyeka umaskini katika bara hilo.

ICC imetoa warka wa kushikwa makamanda watatu waasi Darfur

Luis Moreno Ocampo, Mwendesha Mashitaka wa Mahkama ya UM Juu ya Jinai ya Halaiki (ICC) ametoa hati ya kuwashika makamanda watatu wa vikosi vya waasi wa Darfur, kwa kuhusika na mashambulio yaliofanyika mwezi Septemba mwaka jana katika eneo la Haskanita ambapo walinzi amani 12 wa Umoja wa Afrika waliuawa na 7 walijeruhiwa, na wakati huo huo magari 17 ya UA yalitekwa nyara kambini kwao.