Hapa na Pale

Hapa na Pale

Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP) limefufua tena huduma zake za kiutu katika jimbo la Somaliland, shughuli ambazo zililazimika kusitishwa kufuatia mashambulizi ya mabomu katika mji wa Hargeysa yaliotukia tarehe 29 Oktoba, na moja ya mabomu hayo yalilenga majengo ya ofisi ya Shirika la UM juu ya Miradi ya Maendeleo (UNDP). WFP iligawa tani 522 za chakula katika wiki iliopita, kwa kupitia miradi kadha iliopo nchini kwa sasa.~

KM ameripotiwa, kwa kupitia msemaji wake, ya kuwa bado ana wahka mkubwa kuhusu ya hali ya maisha magumu yaliowakabili wakazi wa KiFalastina wanaoishi kwenye Tarafa ya Ghaza. KM ametilia mkazo kwenye taarifa yake umuhimu kwa serikali ya Israel kuruhusu misaada ya kiutu kuingizwa Ghaza, ili kunusuru maisha ya wakazi wa eneo hilo, na inaelekea mwito wake wa kuyatekeleza hayo haujapewa usikivu wa kuridhisha na wenye madaraka Israel. KM Mdogo Anayehusika na Masuala ya Kiutu na Mshauri wa Misaada ya Dharura, John Holmes, yeye aliyahimiza makundi yote husika na mzozo wa Tarafa ya Ghaza kujizuia na vitendo vya kutumia nguvu, na kupendekeza vituo vya mpakani vifunguliwe haraka, na kwa muda mrefu, ili kuhakikisha misaada ya kihali huwa inawafikia umma muhitaji Ghaza. Alitilia mkazo pia ya kuwa zile “hatua zinazoongeza mateso na shida nyingi, kwa ujumla, dhidi ya wakazi raia katika Ghaza ni lazima zisitishwe, halan, kwa sababu kisheria ni vitendo visiokubalika kamwe.” Holmes alikumbusha KM, mara kwa mara alinakiliwa akishtumu mashambulio ya makombora ya kienyeji yaliolengwa dhidi ya raia wa Israel. Alisema ameshangazwa ya kuwa hadhi ya utu, ubinadamu na hali ya raia wa Ghaza, ambao nusu yao ni watoto wadogo, ni masuala ambayo yamepuuzwa kabisa na makundi yanayohasimiana na mgogoro wa Ghaza.

Kufuatia mashauriano yaliofanyika alasiri Alkhamisi, Baraza la Usalama lilipiisha, kwa kauli moja, azmimio la kuongeza kwa miezi kumi na mbili zaidi, madaraka ya vikosi vya Umoja wa Ulaya vya EUFOR, kuendeleza operesheni zake za kulinda amani katikia Bosnia-Herzegovina. Kadhalika, Baraza la Usalama lilitoa taarifa maalumu kwa waandishi habari, ambayo ilipongeza uchaguzi wa tarehe 16 Novemba katika Guinea-Bissau, uchaguzi ambao uliendelezwa kwa nidhamu na amani.