Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

Hapa na Pale

Alan Doss, Mjumbe Maalumu wa KM kwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (JKK) Ijumaa aliwaambia waandishi habari wa kimataifa waliopo Makao Makuu ya kwamba UM unalazimika kuongeza vikosi vya amani, kidharura, katika taifa hilo, kuzidi ile idadi iliopo sasa hivi ya wanajeshi 19,000. Aliyasema haya baada ya kuripoti mbele ya Baraza la Usalama kuhusu hali ya hatari iliojiri nchini ambayo, alionya, kama haijadhibitiwa mapema kimataifa usalama utateleza na hali kurudia tena “mzozo mbaya sana na wa kutisha” wa taifa. Inakhofiwa mfumko wa mzozo huo utaathiri pia utulivu na amani ya nchi jirani, halkadhalika. Mgogoro wa vita vya wenyewe kwa wenyewe katika JKK, uliochukua miaka sita unakadiriwa kusababisha vifo vya watu milioni 4, ikichanganyika na njaa pia. Mzozo wa JKK umesababisha mauaji makubwa ya watu ambayo hayajawahi kushuhudiwa tangu Vitu Kuu ya Pili ya Dunia kumalizika.

Siku ya Kimataifa kuhishimu watu wa umri mkubwa

Tarehe 01 Oktoba huadhimishwa na UM kama ni Siku Kuu ya Watu Wenye Umri Mkubwa. Siku hii hutumiwa na jamii ya kimataifa kukumbushana umuhimu na ulazima wa kuupatia umma wa watu wakongwe hali njema ya afya, raha, ustawi na hishima, mambo ambayo yameonekana kukosekana katika miaka ya karibuni, licha ya kuwa Mataifa Wanachama yalishaahidi kuondosha ubaguzi dhidi ya fungu hili kubwa, na muhimu, katika jamii zao, umma ambao kila siku hunyimwa haki halali za kimsingi.~~

Hapa na Pale

Zhang Yesui Mjumbe wa Kudumu wa Uchina katika UM atachukua uongozi wa Uraisi wa Baraza la Usalama kwa mwezi Oktoba, baada ya Michel Kafando, Mjumbe wa Kudumu wa Burkina Faso kumaliza muda wa Mwenyekiti wa Baraza kwa mwezi Septemba.

Siku ya Kimataifa Dhidi ya Kutumia Nguvu

Alkhamisi, tarehe 02 Oktoba imeadhimishwa rasmi na UM kuwa ni Siku ya Kimataifa Dhidi ya Kutumia Nguvu, tarehe ambayo inalingana na sikukuu ya kuzaliwa kwa Mahatma Gandhi, kiongozi aliyegombania uhuru wa Bara Hindi kwa kufuata sera ya falsafa alioibuni, yenye kutilia mkazo mapambano ya kutotumia nguvu na wanaokandamiza.

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu awatetea waliowekwa kwenye vifungo onevu

Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu, Navi Pillay, Alkhamisi alifanyisha mahojiano ya awali Geneva na waandishi habari tangu kuanza kazi. Miongoni mwa masuala muhimu aliyoyaangaza na kutilia mkazo zaidi kwenye kikao hicho, ilikuwa ni lile suala linalohusu mradi mpya utakaoanzishwa na ofisi yake unaojulikana kama Mradi wa Kuimarisha Hishima na Haki kwa Watu Waliowekwa Kizuizini.

Kumbukumbu ya majadiliano ya jumla ya Baraza Kuu

AK: Mnamo siku ya mwisho ya majadiliano ya wawakilishi wote, ya kikao cha 63 cha Baraza Kuu la UM, yaliofanyika Ijumatatu, viongozi kadha wa kadha wa dunia walibaini kwenye hotuba zao kwamba wangelipendelea kuona UM unatumiwa kuwa ni chombo imara cha kimataifa, kupunguza mivutano kati ya Mataifa Makuu ili kuhakikisha kunakuwepo uwiano wa masilahi yenye natija kwa nchi ndogo vile vile, mataifa ambayo mahitaji yao ni lazima yapewe umuhimu unaofaa kwa ajili ya utulivu na amani ya ulimwengu mzima.~