Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kumbukumbu ya majadiliano ya jumla ya Baraza Kuu

Kumbukumbu ya majadiliano ya jumla ya Baraza Kuu

AK: Mnamo siku ya mwisho ya majadiliano ya wawakilishi wote, ya kikao cha 63 cha Baraza Kuu la UM, yaliofanyika Ijumatatu, viongozi kadha wa kadha wa dunia walibaini kwenye hotuba zao kwamba wangelipendelea kuona UM unatumiwa kuwa ni chombo imara cha kimataifa, kupunguza mivutano kati ya Mataifa Makuu ili kuhakikisha kunakuwepo uwiano wa masilahi yenye natija kwa nchi ndogo vile vile, mataifa ambayo mahitaji yao ni lazima yapewe umuhimu unaofaa kwa ajili ya utulivu na amani ya ulimwengu mzima.~

AK:Nkosazana Dlamini Zuma, Waziri wa Nchi za Nje wa Afrika Kusini alisema kutokuwepo kwa mjumbe wa kudumu wa Afrika kwenye Baraza la Usalama ni “mzaha wenye kukejeli haki halali ya kimataifa” hasa ilivyokuwa kazi kuu inayoendelezwa katika Baraza hilo la wajumbe 15 inahusika zaidi na masuala ya Afrika. Alipendekeza uwanachama wa Baraza la Usalama uongezwe, ikiwa miongoni mwa mapendekezo ya kuleta “mageuzi ya kimsingi” kwenye kazi za Umoja wa Mataifa, na katika zile taasisi za kifedha zinazojulikana kama taasisi za Bretton Woods, ikijumlisha Benki Kuu ya Dunia, na vile vile kuleta marekibisho kwenye mashirika mengine ya kimataifa. Bi Dlamini Zuma alisisitiza masuala magumu yanayoukabili ulimwengu wetu sasa hivi – kama migogoro ya fedha, mzozo wa kupanda kwa kasi kwa bei za mafuta kwenye soko la kimataifa na pia bei za juu za chakula – ni masuala ambayo hayatoweza kutatuliwa kwa haki pindi “mataifa mengi bado yanaendelea kunyimwa fursa ya kushiriki kwenye maamuzi yenye kuongoza utawala wa dunia, kwenye taasisi za kimataifa.’

AH:Mjumbe wa Libya katika Baraza Kuu, Giadalla A. Ettalhi risala yake kwenye kikao cha 63 cha Baraza Kuu ilionya ya kuwa utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia katika Afrika unazorota kwa sababu ya vizingiti vinavyotokana na ulaji rushwa, mirungura, na uhamishaji haramu wa fedha nje, hasa zile pesa zilizopatikana kwa njia isio halali. Ettalhi, mwenyekiti wa ujumbe wa Libya katika UM, alitilia mkazo kwenye risala yake kwamba “madhara makubwa huzisibu nchi zinazoendelea kwa sababu ya biashara ya magendo ya kuhamisha fedha zilizoibiwa ndani ya nchi, ambazo hupelekwa nje na kuhifadhiwa kwenye akaunti ya akiba ya siri.” Alisema angelipendelea kuona hatua kali zinachkuliwa kimataifa dhidi ya vile vituo vya biashara vyenye kuhifadhi fedha hizo, na kuhakikisha fredha zilizotoroshwa kwa njia zisio za kisheria zinarejeshewa taifa husika liliopoteza mali hiyo.

AK:Mjumbe wa Kudumu wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kogno katika UM, Ileka Atoki alitoa mwito maalumu uitakayo walinzi wa amani wa UM wapewe madaraka zaidi, yalio wazi ikichanganyika na uwezo wa kutumia nguvu, pindi ikiwezekana, ili kurudisha utulivu na amani katika nchi. Alivitaka vikosi vya UM vitumiwe, haraka iwezekanavyo, kukomesha uchokozi na vurugu linalopaliliwa na waasi wa kundi la CNDP, waasi ambao vitendo vyao vinayanyima majimbo ya mashariki matunda ya amani, usalama na ujenzi mpya wa maendeleo. Alisema mapigano ya karibuni katika maeneo ya mashariki yalisababisha idadi kubwa ya raia kuhama makazi ili kunusuru maisha.

AH:Osman Saleh, Waziri wa Nchi za Kigeni wa Eritrea aliliambia Baraza Kuu “sera za kukandamiza zenye kushauriwa vibaya” za Marekani ndio zenye kusababisha na kukithirisha mizozo mbalimbali katika dunia, na kuathiri vibaya biashara ya fedha, hali za kiutu na huduma za uchumi kwa ujumla. Alidai mwelekeo wa sera ya Marekani humaanisha “uongozi wa mizozo”, na alitoa mfano wa mzozo ulioselelea kati ya Ethiopia na Eritrea, mapigano na maafa ya kiutu yaliolivaa taifa la Usomali, vurugu katika Sudan, na mapigano yakaribni kati ya Ethiopia na Eritrea kuwa ni mifano ya mizozo ambayo ama ilianzishwa na Washington, au iliendelezwa nayo au suluhu ya kuridhisha ilizingiwa na kuzuiliwa na Marekani.

AK:Seyoum Mesfin,Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ethiopia yeye alisema ni muhimu kwa UM kutekeleza marekibisho na mabadiliko kwenye mfumo wa kazi zake kama inataka kuendelea kuaminiwa kwa ridhaa ya Mataifa Wanachama yote, na kwa ajili ya maadili yenye kuongoza kazi za taasisi hii, katika siku za usoni, taasisi ambayo inahusisha washiriki wingi sana wa kimataifa. Alisema UM ndio “mlezi wa diplomasiya ya wahusika wingi” na hakuna kipindi tangu Vita Kuu ya Pili kumalizika, ambapo umma wa kimataifa unahitajia kidharura chombo cha kukabiliana na matatizo ya kimataifa, kwa ushirikiano wa dhati na uhusiano wa washirika wingi, kama kipindi cha hivi sasa.