Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

UM umeahidi kuisaidia Uchina kukabiliana na athari za zilzala

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti kwamba imeitumia Serikali ya Uchina barua maalumu ilioahidi kwamba UM umejiandaa kupeleka wataalamu wanaohusika na huduma za haraka za maafa ili kuchangia juhudi za kuwasaidia, kihali na mali, waathiriwa wa zilzala iliopiga eneo la kusini-magharibi ya Uchina Ijumanne. Zilzala hiyo, tumearifiwa, imeshauwa maelfu ya watu, idadi ambayo inakhofiwa huenda ikaongezeka kwa kima kikubwa kabisa baadaye.

Mkuu wa UNHCR atazuru Yemen kuzingatia hifadhi imara kwa wahamiaji wa Usomali na Ethiopia

Antonio Guterres, Kamishna Mkuu wa Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) Ijumatano ataanza ziara ya siku tano nchini Yemen, kushauriana na Serikali pamoja na wahisani wa kimataifa juu ya taratibu za kuchukuliwa shirika za kuwapatia wahamiaji wa Usomali na Ethiopia waliopo Yemen hifadhi bora. Guterres anatazamiwa pia kuhudhuria Mkutano wa Kikanda wa siku mbili juu ya Hifadhi ya Wahamiaji na Udhibiti Bora wa Uhamiaji wa Kimataifa, hususan lile fungu la raia waliotokea Pembe ya Afrika, mkutano utakaofanyika Sana\'a, Yemen kuanzia tarehe 19 hadi 20 Mei.

ITU imeripoti kukithiri kwa wateja wa simu za mkononi Afrika

Hamadoun Toure, Katibu Mtendaji wa Shirika la UM juu ya Mawasiliano ya Kisasa (ITU) ambaye hivi sasa yupo Cairo, Misri akihudhuria maonyesho ya maendeleo ya viwanda vya mawasiliano, alinakiliwa akisema kwamba mnamo miaka mitatu iliopita bara la Afrika liliongoza katika matumizi ya huduma za mawasiliano ya simu. Kwa mujibu wa ripoti za ITU huduma za sekta ya simu katika Afrika ziliongezeka kwa kiwango kisichotarajiwa, mathalan, mwaka jana watu milioni 65 walisajiliwa kuwa wateja wapya wa simu za mkononi.

Myanmar yanasihiwa kurahisisha huduma za msingi kwa waathiriwa wa kimbunga

Ijumatatu mjini Bangkok, Thailand, kwenye mkutano wa mashirika ya UM na waandishi habari juu ya misaada ya dharura kwa Myanmar, kulitolewa onyo na UM lenye kuitahadharisha Serikali ya Myanmar ya kuwa idadi kubwa ya raia huenda ikaangamia kwenye maeneo yalioharibiwa na Kimbunga Nargis pindi wenye madaraka hawatorahisisha uwezo wa wataalamu wa kimataifa wanaohudumia misaada ya dharura, kuwafikia, haraka, waathiriwa wa maafa ya tofani, ambao wametawanyika katika sehemu mbalimbali za nchi.

Kucheleweshwa vibali vya misaada ya kiutu Myanmar kwaisumbua UM

KM Ban Ki-moon alikutana na waandishi habari wa kimataifa kwenye Makao Makuu ambapo aliwapatia taarifa mpya kuhusu operesheni za mashirika ya UM za kupeleka misaada ya kiutu katika Myanmar, kwa umma ulioathirika na Kimbunga Nargis kilichogharikisha sehemu kadha za nchi mnanmo tarehe 02 Mei. KM alisema mashirika ya kimataifa yamekadiria watu milioni 1.5 wamo ukingoni hatari wa kuangamia pindi misaada ya kimataifa itaendelea kucheleweshwa kuwafikia kwa sababu ya vizingiti vya kirasimu vilivyowekwa na wenye mamlaka nchini humo.

Tume ya kudhibiti mifumko ya bei ya chakula ulimwenguni inakutana Makao Makuu

Ijumatatu asubuhi KM Ban Ki-moon aliongoza, kwa mara ya kwanza, mashauriano muhimu na wawakilishi wa tume maalumu iliodhaminiwa madaraka ya kuandaa ajenda ya mkutano mkuu utakaofanyika mwezi ujao mjini Roma, Utaliana kuzingatia hatua za kuchukuliwa na Nchi Wanachama, kudhibiti bora tatizo la mifumko ya bei za nafaka kwenye soko la kimataifa. Tume inajumuisha mashirika yote ya UM yanayohusika na shughuli za maendeleo na misaada ya kiutu, na pia Benki Kuu ya Dunia, Shirika la Fedha la Kimataifa na Shirika la Biashara Duniani (WTO).

Mavuno ya mpunga yanabashiriwa muongezeko mkubwa katika 2008

Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) limeripoti kwamba mavuno ya mpunga katika mataifa ya Asia, Afrika na Amerika ya Latina yataongezeka kwa asilimia 2.3 katika 2008, muongezeko ambao utakiuka tani milioni 600 ziada. Hata hivyo bei ya mchele katika soko la kimataifa inakhofiwa itaendelea kuwa ya kiwango cha juu kabisa, kwa sababu nafaka hizo hazitomalizika kuvunwa mpaka mwisho wa mwaka.

Mkataba wa Kulinda Haki za Walemavu unasherehekewa na Baraza Kuu

Baraza Kuu la UM lilikusanyika kwenye Makao Makuu kwenye sherehe maalumu ya kuwaheshimu na kuwatambua wale wajumbe wajasiri wa kutoka Serikali Wanachama kadha, wakichanganyika na jamii ya watu walemavu pamoja na watumishi wa Taasisi kadha wa kadha za UM, kwa juhudi zao za muda mrefu ambazo zilifanikiwa kuwasilisha Mkataba mpya wa Kimataifa juu ya Haki za Watu Wenye Ulemavu pamoja na Itifaki ya Khiyari. Karibuni Mkataba wa Walemavu Duniani uliidhinishwa rasmi kuwa chombo cha sheria ya kimataifa, na utatumiwa kudhamini na kulinda haki za walemavu milioni 650 wanaoishi katika sehemu mbalimbali za ulimwengu.

KM ashtumu vikali vurugu liliozuka Khartoum mwisho wa wiki

KM Ban Ki-moon "ameshtumu vikali vitendo vya kutumia mabavu vilivyoendelezwa na jeshi la mgambo la kundi la JEM kwenye vitongoji vya mji mkuu wa Khartoum, Sudan" mnamo mwisho wa wiki. Kwa mujibu wa taarifa iliotolewa na msemaji wa KM Ban, ilisisitizwa ya kwamba utumiaji mabavu na makundi yenye silaha kusuluhisha tatizo la kisiasa ni kitendo kisiokubalika na jamii ya kimataifa kuitatua migogoro iliokabili Sudan sasa hivi, hasa ilivyokuwa vitendo hivyo vinahatarisha zaidi usalama na amani ya raia.

Jee, sekta ya utalii Kenya ina matumaini ya kufufuka?

Baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu kutangazwa Kenya mnamo Disemba 30, 2007 kulizuka machafuko ya kushhtusha yaliosambaa katika sehemu mbalimbali za nchi. Wiki chache tu kufuatia machafuko hayo mashirika ya kimataifa yaliripoti kwamba watu 1,500 waliuawa na raia 300,000 walilazimika kuhama mastakimu yao ili kunusurisha maisha. Watu hawa walipatiwa makazi ya muda na wenye madaraka, mbali na makwao.