Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

WHO inahimiza mataifa yazingatie haraka udhibiti wa maradhi yanayoua watoto kwa wingi

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetoa ripoti yenye kuihimiza jamii ya kimataifa kuendelea kuhudumia shughuli zinazohusika na udhibiti bora wa magonjwa ya kuambukiza yanayoumiza zaidi watoto wachanga, hususan ile homa ya vichomi na maradhi ya kuharisha. Mwito huu ulitolewa baada ya kugundulikana katika kipindi cha karibuni mchango mkubwa wa huduma za afya umeonekena ukitumiwa kwenye shughuli za kudhibiti UKIMWI, kifua kikuu na malaria na yale maradhi ya kuambukiza yenye kuathiri zaidi watoto yameonekana kutengwa na kutopewa umuhimu unaostahiki.

BU kupitisha azimio kwa UNMIS kuendeleza shughuli za amani Sudan

Baraza la Usalama limepitisha maazimio kadha yanayohusu shughuli za ulinzi wa amani katika Bara la Afrika.~Awali, Ijumatano wajumbe wa Baraza la Usalama walipitisha, kwa kauli moja, azimio lilioahidi kuendelea kuunga mkono Mapatano ya Jumla ya Amani ya 2005 ya kusitisha uhasama, kati ya Sudan kaskazini na kusini, maafikiano ambayo utekelezaji wake unasimamiwa na kufuatiliwa na Shirika la UM la Ulinzi wa Amani Sudan Kusini (UNMIS). Azimio limependekeza shughuli za UNMIS ziendelezwe Sudan mpaka Aprili 30, 2009.

MINURSO imeongezewa muda na BU kutuliza hali Sahara Magharibi

Baraza la Usalama pia limepitisha, kwa pamoja, azimio la kuongeza muda wa kazi za Shirika la MINURSO katika eneo la Sahara ya Magharibi hadi Aprili 30 mwakani. MINURSO ni shirika la ulinzi wa amani la UM, liliodhaminiwa madaraka ya kufuatilia kusitishwa kwa hali ya mapigano baina ya Morocco na Chama cha Wazalendo wa Sahara Magharibi cha Frente Polisario. Vile vile MINURSO inatarajiwa kutayarisha mazingira yanayoridhisha ili kuweze kufanyika kura ya maoni kwenye eneo hilo la Afrika Kaskazini.

Kamati ya Habari inakutana Makao Makuu kwenye kikao cha mwaka

Kamati ya Baraza Kuu juu ya Masuala ya Habari ilianza mijadala ya mwaka mapema wiki hii katika Makao Makuu ya UM. Naibu KM kuhusu Mawasiliano na Habari kwa Umma, Kiyo Akasaka aliwaambia wajumbe wa Kamati kwamba UM unatakiwa kupatiwa ushirikiano mzuri zaidi, na wa kutegemewa, kutoka Mataifa Wanachama, ili tuweze kuhakikisha “tunatekeleza, kama ipasavyo, marekibisho yenye natija kwa umma wa kimataifa.”

Sikukuu ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani itaadhimishwa Mei tatu

Tarehe 03 Mei huadhimishwa kila mwaka na jamii ya kimataifa kuwa ni SikuKuu ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani. Idara ya Habari kwa Umma ya UM (DPI) pamoja na Shirika la UM juu ya Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) yameandaa tafrija mbalimbali kuwakumbusha walimwengu juu ya umuhimu, na pia ulazima, wa kuwa na vyombo vya habari vilivyo huru.

SikuKuu ya Wafanyakazi Duniani

Ilivyokuwa leo ni Mei Mosi nachukua fursa hii kuwatakia wasikilizaji wetu wote wa Idhaa ya Kiswahili ya UM, pote walipo ulimwenguni, kheri na fanaka wakati wanaiadhimisha Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani.