Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

Usomali kupwelewa kuandikisha watoto wa skuli za msingi, imeonya UNICEF

Veronique Taveau, Msemaji wa UNICEF mjini Geneva aliwaambia waandishi habari Ijumaa kwamba taifa la Usomali lina sifa mbaya ya uandikishaji mdogo kabisa wa watoto wanaohudhuria skuli za msingi, hususan watoto wa kike. Hivi sasa imebainishwa kwamba idadi ya watoto wa kike wanaohudhuria skuli za msingi nchini ni 121,000. UNICEF impenedekeza idadi hiyo iongozwe mara mbili katika 2009 na wanalenga kuwapatia watoto wa kike 50,000 fursa ya kuhudhuria skuli za msingi mwakani.~~

Hapa na pale

Ofisi ya Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu Geneva, imetangaza ya kuwa Louise Arbour ameamua kustaafu mwezi Juni atakapomaliza miaka minne ya mkataba wake wa kazi. Arbour angelipendelea kuendelea kuongoza ofisi hiyo, na kuwakabili kinaga naga wale wakosoaji dhidi yake, lakini alisema anaaamini wakati umefika kushughulikia zaidi mahitaji ya familia yake sasa hivi.

Uhamisho wa dharura bado waendelea Mogadishu

William Paton, Mshauri Mkaazi wa UM kuhusu Misaada ya Kiutu kwa Usomali ameripoti kuwa na wasiwasi juu ya hali ya raia 200,000 waliong’olewa makwao kutoka mji wa Mogadishu kwa sababu yaukosefu wa sualama. Kwa mujibu wa takwimu za UM, katika Januari na Februari mwaka huu wahamiaji 25,000 walikuwa wakihajiri mji kila mwezi na kumiminikia kwenye barabara inayoelekea eneo la Afgooye, ambapo kumefumka makazi ya muda ya huku na kule zaidi ya mia moja.

Hali katika Kenya na Usomali yasailiwa na BU

Ijumatano Baraza la Usalama lilikutana kushauriana hatua za kuchukuliwa na jumuiya ya kimataifa ili kurudisha utulivu na amani katika Usomali. Kadhalika Baraza lilisailia hali, kwa ujumla, nchini Kenya baada ya wajumbe wa taasisi hiyo kusikiliza fafanuzi ya ripoti ya Haile Menkerios, Msaidizi wa KM juu ya Masuala ya Kisiasa. ~~~

Rwanda yakubali kupokea wahalifu waliohukumiwa na ICTR

Mapema wiki hii mjini Kigali, Adam Deng, Msajili wa Mahakama ya UM juu ya Rwanda (ICTR) pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, walitia sahihi maafikiano ya kupeleka kifungoni kwenye magereza ya Rwanda wale watu waliohukumiwa adhabu na Mahakama. Rwanda itakuwa ni taifa la saba kuidhinisha huduma ya kuweka vizuizini wale watu waliohukumiwa na Mahakama ya ICTR kushiriki kwenye jinai ya halaiki katika Rwanda.

Hapa na pale

Bodi la Utawala la Shirika la UM juu ya Haki za Wafanyakazi wa Kimataifa (ILO) leo limeanza kikao chache cha 301, ambapo miongoni mwa masuala yatakayozingatiwa itajumuisha utekelezaji wa haki za kimsingi za ajira katika baadhi ya nchi, ushirikiano kati ya sekta za binafsi na kiraia, pamoja na kusailia shughuli za ILO za kuwasaidia wafanyakazi wahamiaji na udhibiti ubaguzi dhidi yao. ~

Operesheni za awali za Polisi wa UNAMID zaanzishwa rasmi Darfur Kaskazini

Ikiwa miongoni mwa juhudi za kuimarisha ushirikiano bora na hali ya kuaminiana, baina ya Umoja wa Mataifa pamoja na wenyeji na polisi katika Darfur, operesheni za kwanza za polisi wa Vikosi Mseto vya UM/UA kwa Darfur (UNAMID) zilianzishwa mapema wiki hii katika sehemu za Darfur ya Kaskazini kujenga imani. Eneo hili linasimamiwa na kundi la Mini Minawi, tawi la wanamgambo waasi wa SLA.