Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

BU lazingatia ujenzi wa amani Guinea-Bissau

Baraza la Usalama (BU) limekutana, kwanza, kwenye kikao cha hadhara kuzingatia hali katika Guinea-Bissau, kufuatia ripoti ya karibuni ya KM iliyosailia hatua za kuchukuliwa kimataifa kulisaidia taifa hili la Afrika Magharibi kufufua tena huduma zake za maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na pia kijamii. Mwakilishi wa KM katika Guinea-Bissau, Shola Omoregie aliwaelezea wajumbe wa Baraza kwamba Ijumanne (25 Machi) usiku Raisi Vieira ametangaza kwamba Guinea-Bissau itafanya uchaguzi wa Baraza la Kutunga Sheria mnamo tarehe 16 Novemba. Tangazo hili, aliendelea kusema, linatarajiwa kuteremsha hali ya wasiwasi iliyolivaa taifa katika siku za karibuni, na alitumai washirika wenzi kutoka jumuiya ya kimataifa wataifadhilia Guinea-Bissau misaada inayohitajika kuendesha uchaguzi kwa utaratibu wa kuridhisha.

Uchanganuzi batini wa Tanzania juu ya kikao cha Kamisheni ya Maendeleo ya Jamii

Kuanzia tarehe 06 mpaka 15 Februari wawakilishi wanachama wa Kamisheni juu ya Maendeleo ya Jamii walikusanyika kwenye Makao Makuu ya UM mjini New York, kuhudhuria kikao cha mwaka, cha arobaini na sita, ambapo walizingatia mada maalumu zenye kuhusu masuala yanayoambatana na huduma za jamii, mathalan, taratibu za kukuza ajira, nidhamu ya kukidhi vyema mahitaji ya umma unaozeeka pamoja na kusailia matatizo yaliowakabili walemavu ulimwenguni.

Mafanikio ya kukomesha maradhi ya polio Usomali

Taasisi Inayohusika na Mradi wa Kuondosha Maradhi ya Kupooza/Polio Duniani (GPEI) imetangaza ya kuwa walimwengu, wiki hii, wamefikia ‘mafanikio ya kihistoria’ kuhusu afya ya jamii nchini Usomali, baada ya kubainika kwamba tangu tarehe 25 Machi 2007 hakujasajiliwa mgonjwa hata mmoja aliyeambukizwa na virusi vya maradhi ya polio katika taifa hilo.

'Polio yaweza kudhibitiwa sehemu zote za dunia', asisitiza Mkurugenzi wa WHO

Mkurugenzi wa Ofisi ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa Ukanda wa Mediterranean ya Mashariki, Dktr Hussein Gezairy amenakiliwa akisema ya kuwa “mafanikio ya huduma za kuondosha polio Usomali yamethibitisha kwamba maradhi haya yanaweza kukomeshwa katika sehemu zote za dunia, hata kwenye yale maeneo yalioshuhudia vurugu na uhasama”, pindi jumuiya ya kimataifa itanuia kushirikiana kipamoja kuitekeleza miradi hiyo ya kudhibiti afya ya jamii. Hivi sasa ni mataifa manne tu duniani ambayo bado yanasumbuliwa na tatizo la polio ulimwenguni – mataifa hayo ni Afghanistan, India, Nigeria na Pakistan.

Vurugu la Mashariki ya Kati laitia wasiwasi Baraza la Usalama

Baraza la Usalama limekutana kwenye kikao cha hadhara Ijumanne kuzingatia na kusailia hali inayoendelea kuharibika katika Mashariki ya Kati. Naibu KM juu ya Masuala ya Kisiasa, Lynn Pascoe alipohutubia Baraza la Usalama aliwaambia wajumbe wa taasisi hiyo kwamba tangu alipowakilisha ripoti yake mwezi uliopita, kuhusu hali ardhini katika eneo zima la Mashariki ya Kati, juhudi za upatanishi zimeonekana kupwelewa, kwa sababu ya kuongezeka kwa vitendo vya utumiaji nguvu ambavyo vilisababisha idadi kubwa ya raia kujeruhiwa na kuuawa, hususan kwenye yale maeneo yaliokaliwa kimabavu katika Tarafa ya Ghaza, Ufukwe wa Magharibi ya Mto Jordan, baadhi ya maeneo ya Israel na nchini Lebanon.~

UM inawakumbuka wafanyakazi walioghibiwa na hali ya hatari

Tarehe 25 Machi hutambuliwa na UM kuwa ni Siku ya Ushikamano wa Kimataifa Kuwakumbuka Wafanyakazi wa UM, Waume kwa Wake, Waliowekwa Vizuizini na Waliopotea wakati wakitumikia “maadili ya kiutu” katika sehemu mbalimbali za dunia. Risala ya KM kuadhimisha siku hii ilidhihirisha kwamba wafanyakazi wa UM 40, wingi wao wakiwa wazalendo, wameripotiwa kuwekwa vizuizini katika mataifa mbalimbali, na wengine wamekamatwa na baadhi yao wamepotea na kutoweka bila kujulikana walipo au walipohamishiwa. ~~

UNICEF imelaani utekaji nyara wa wahandisi Darfur Kaskazini

Shirika la Umoja wa Mataifa juu ya Mfuko wa Maendeleo ya Watoto (UNICEF) limelaani kitendo haramu cha utekaji nyara katika eneo la Um Tajok, Darfur Kaskazini, na kutorosha kundi la wahandisi wanne wanaotumikia Shirika la Maji la Taifa Sudan pamoja na madereva wao wanne, na pia magari na vifaa vya kuchimbia maji.