Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashirika ya UM yanaendelea kuhudumia misaada ya kiutu Kenya

Mashirika ya UM yanaendelea kuhudumia misaada ya kiutu Kenya

Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) linaendeleza operesheni za kuwahamisha wahamiaji 6,500 wa Kenya waliokwama kwenye miji ya mipakani ya Busia na Malaba na kuwapeleka katika eneo la Mulanda, liliopo Uganda ya kati, ili kukidhia mahitaji yao ya kihali. Uhamisho huu ulilazimika ufanyike kwa sababu hali ya usalama, tuliarifiwa, ilizidi kuharibika nchini Kenya. ~

Shirika la UM juu ya Makazi (UN-HABITAT) limetuma timu ya uchunguzi kutathminia hali na kuthibitisha jumla ya watu waliomiminikia kwenye zile kambi za wahajiri wa ndani ya nchi (IDPs), ikijumuisha pia zile kambi za IDPs za Nairobi na Eldoret. Vile vile timu ya UN-HABITAT itaendeleza uchunguzi ziada kuhusu safi na maji salama kwenye kambi za IDPs. Wakati huo huo Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo ya Watoto (UNICEF) linawahudumia watoto wadogo waliopo kwenye kambi zote za IDPs Kenya, chanjo kinga dhidi ya shurua na maradhi ya kupooza (polio). Halkadhalika, Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP), kwa ushirikiano na wenye madaraka Kenya, pamoja na Jumuiya ya Msalaba Mwekeundu Kenya (KRCS) wameanza kugawa misaada ya chakula cha mwezi kwa watu muhitaji 67,000 waliopo Eneo la Bonde la Ufa (Rift Valley), na pia kuanzisha operesheni za kuhudumia chakula wakazi wa mitaa ya mabanda mjini Nairobi.