Skip to main content

Hapa na pale

Hapa na pale

Shirika la Haki za Wafanyakazi wa Kimataifa (ILO) limetoa ripoti mpya yenye kuzingatia ‘Mwelekeo wa Ajira Duniani kwa 2008’ na kuonya kwamba kwa kulingana na takwimu za ILO watu milioni 5 watanyimwa ajira mwaka huu kwa sababu ya kutanda kwa misukosuko ya uchumi, ambayo huchochewa na machafuko kwenye soko la mikopo, pamoja na mfumko wa bei za mafuta katika soko la kimataifa.~

Kadhalika Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo ya Watoto (UNICEF) limewasilisha ripoti ya mwaka inayosalia "Hali ya Watoto Duniani katika 2008 – Vipi Tuwanusuru?”; ripoti ambayo imetilia mkazo umuhimu wa mataifa kuekeza zaidi kwenye sekta ya afya ya watoto wadogo na mama, ili kupunguza vifo vya watoto 25,000 chini ya umri wa miaka mitano ambavyo hujiri kila siku duniani kwa sababu ukosefu wa huduma za kutunza afya.

Taasisi ya UM ya Kupunguza Athari za Maafa ikijumuika na Shirika la Afya Duniani (WHO), na Benki Kuu ya Dunia zimeanzisha kampeni maalumu ya kimataifa kutokea mji wa Davos, Uswiss iliokusudiwa kuhakikisha mahospitali yatatunzwa na kupatiwa usalama unaofaa wakati maafa ya kimaumbile yanapojiri ulimwenguni, hali ambayo mara nyingi huwanyima mamilioni ya umma huduma za dharura za afya.

Joseph Domensch, Ofisa Mkuu wa Uganga wa Mifugo katika Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) ameonya kwamba ijapokuwa tulifanikiwa katika miezi ya karibuni kudhibiti virusi vya H5N1 vinavyosababisha homa ya mafua ya ndege, hata hivyo janga hili bado linaendelea kuhatarisha afya ya kimataifa, hususan baada ya maradhi haya kugunduliwa karibuni katika zaidi ya darzeni za nchi.

Baraza la UM juu ya haki za Binadamu lilipokutana Alkhamisi Geneva lilipitisha azimio lenye kuitaka jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za dharura dhidi ya Israel ili ikomeshe, halan, ukiukaji uliovuka mpaka wa haki za kiutu kwenye Ardhi Iliokaliwa Kimabavu ya Wafalastina, na vile vile kuitaka Israel kuhudumia haraka umma muathiriwa wa eneo hilo chakula, madawa, nishati na pia uhuru wa kutembea.

KM Ban Ki-moon alisema kwenye risala alioiwakilisha mbele ya wajumbe waliohudhuria Mkutano Mkuu Kuzingatia Uchumi wa Dunia kwenye mji wa Davos, Uswiss kwamba mtihani mkubwa ulioikabili jumuiya ya kimataifa ni ule unaohusiana na tatizo la kudhibiti bora maji mingi, yalio safi na salama ili kutumiwa na umma wote kote duniani.