Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Habari kwa Ujumla

Watendaji wa UM wawasili Aleppo, uhamishaji raia warejea

Kazi ya kuondoa raia kutoka Aleppo nchini Syria ambako mapigano yameshika kasi, imeanza tena baada ya kusitishwa kwa zaidi ya siku moja huku watendaji 20 wa Umoja wa Mataifa wakiwasili eneo hilo kuhakikisha uhamaji wao unakuwa salama.

Hatua hiyo imekuja baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupitisha azimio siku ya Jumatatu lililoridhia kupelekwa kwa watendaji  hao wa Umoja wa Mataifa.

AMISOM kurejesha serikalini chuo chake cha Taifa Somalia

Ujumbe wa Muungano wa Afrika nchini Somalia AMISOM uko mbioni kukamilisha mipango ya kukabidhi Chuo Kikuu cha Taifa cha Somalia kwa serikali ya nchi hiyo.

Katika taarifa yake AMISOM imesema hadi hivi karibuni chuo hicho kilikuwa chini ya uongozi wake kwa zaidi ya nusu muongo, kikitumiwa na jeshi la Burundi kama makao yake makuu.

Makubaliano ya kukabidhi chuo hicho yalifikiwa hivi karibu baada ya maamuzi ya kuhamishia kikosi cha Burundi Johwar kufikiwa.

Amani izingatiwe kwenye kipindi cha mpito DRC- Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema anafuatilia kwa karibu hali inavyoendelea huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC wakati huu ambapo usuluhishi unaoongozwa na mkutano wa kitaifa wa makanisa nchini huko CENCO umeanza tena hii leo.

Taarifa ya msemaji wake imemnukuu Katibu mkuu akizitaka pande zote zinazohusika katika upatanishi na usuluhishi kuafikiana kwa njia ya amani na kujaribu kutatua masuala yanayohusiana na mipango ya mpito kuelekea uchaguzi mkuu kwa mujibu wa katiba ya DRC.

Kauli za Duterte kuwa aliua watu zichunguzwe: Zeid

Kamishna wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad Al Hussein ametoa wito kwa mamlaka ya mahakama ya Ufilipino kuzindua mchakato wa uchunguzi kufuatia tamko la wiki iliyopita la Rais Rodrigo Duterte wa Ufilipino kuwa wakati akiwa Meya wa Davao aliua watu na kushawishi watu wengine wafanye hivyo.

Rais Duterte alinukuliwa tarehe 14 mwezi huu akieleza kuwa wakati akiwa meya alifanya doria usiku kwa kutumia pikipiki na kuuawa watu ambapo alienda mbali zaidi na kuthibitisah kuua watu watatu.

Misaada ya vyakula yaanza kuwafikia wakazi wa Aleppo

Baada ya vuta nikuvute baina ya pande kinzani nchini Syria juu ya kuruhusu watoa misaada ya kibinadamu mjni Aleppo, mji unaotajwa kuathirika zaidi na mzozo nchini humo, hatimaye wakazi wa mji huo hususani Mashariki wameona nuru kwa kupata misaada ya vyakula.

Umoja wa Mataifa umeanza operesheni ya kugawa vyakula katika mji huo ambao umezingirwa na vikosi vyenye silaha. Joseph Msami amemulika kuanza kwa ugawaji huo na hii hapa ni taarifa yake.

Magaidi husafirisha watu na kutekeleza ukatili wa kingono, tuchukue hatua-Ban

Baraza la usalama leo limekuwa na mjadala wa ngazi ya mawaziri kuhusu usafirishaji haramu wa watu katika maeneo yenye mizozo, mada inayohusiana na kulinda amani ya kimataifa na usalama.

Akizungumza katika majadala huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema licha ya kwamba usafirishaji haramu unavuka mipaka, waathirika zaidi ni wale walioko katika mizozo hususani wanawake, watoto, wakimbizi wa ndani na wakimbizi.

Ban amesema magaidi hutumia mwanya huo kuchomoza na kutesa watu huku akitolea mfano.

(Sauti Ban)

UN Photo/Loey Felipe

Ban atuma salamu za rambirambi kufuatia shambulio la ugaidi Ujerumani

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ametuma salamu za rambirambi kufutia vifo vya watu 12 baada ya shambuliolinalodaiwa kuwa la kigaidi mjini Berlin Ujerumani

Polisi mjini humo wanasema ajali ya lori lililoacha njia na kuvamia soko maarufu kwa maandalizi ya krisimasi ilikuwa ya makusudi .

Taarifa ya msemaji wa Ban, imemnukuu Katibu Mkuu akizipa pole familia zilizopoteza wapendwa wao katika tukio hilo, serikali na watu wa Ujerumani pamoja na kuwatakia majeruhi uponyaji.

Chukueni hatua sasa kuokoa wananchi wa Sudan Kusini- Ban

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na kikao kuhusu Sudan Kusini ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema wananchi wamekata tamaa na tegemeo lao lililosalia kwa jamii ya kimataifa linazidi kuyoyoma.

Akihutubia wajumbe wa Baraza hilo Ban amesema ukosefu wa usalama, njaa, uchumi kutwama ni sehemu tu ya madhila yanayokumba wananchi hao licha ya matumaini  waliyokuwa nayo baada ya kupata uhuru mwaka 2011.

Balozi wa Urusi nchini Uturuki auawa, UM walaani

Balozi wa Urusi nchini Uturuki Andrey Karlov ameuawa kwenye mji mkuu Ankara.

Vyombo vya habari vinaripoti kuwa mtu mmoja aliyekuwa na silaha alimpiga risasi balozi Karlov jumatatu jioni kwa saa za Uturuki wakati wa maonyesho , ambapo hata hivyo mtu huyo yaripotiwa aliuawa na maafisa wa polisi.

Ban kupitia taarifa ya msemaji wake amelaani kitendo hicho akituma salamu za rambirambi kwa familia ya balozi Karlov na serikali ya Urusi.