Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nambari 109 yaokoa maisha yangu- Egide

Mfumo wa kupiga simu namba 109 umesaidia kuokoa watu wanaotumbukia kwenye vitendo vya utekwaji nyara nchini Burundi. (Picha:https://goo.gl/c3Zwnz)

Nambari 109 yaokoa maisha yangu- Egide

Nchini Burundi mfumo wa kupiga simu wakati wa dharura umeokoa maisha ya wengi akiwemo mwananchi mmoja ambaye alitekwa mwezi Aprili mwaka huu.

Egide ambaye si jina lake halisi alinusurika mikononi mwa watekaji wake baada ya mkewe kutumia mfumo huo wa kupiga simu namba 109 unaotoa fursa ya jamii kupiga simu pindi inapokabiliwa na dharura.

Wahudumu wa mfumo huo waliweza kusaka mbinu za kuzungumza na wateka nyara wa Egide na ndipo alipoachiliwa huru siku 10 baadaye na kutelekezwa karibu na mto mpakani mwa Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Shirika la uhamiaji duniani, IOM ambalo ni miongoni mwa wadau walioanzisha mfumo huo kufuatia mzozo wa kisiasa nchini Burundi, wamesema watekaji nyara wa Egide ni miongoni mwa vikundi vilivyojihami ambavyo hutumia pesa zinazolipwa kumkomboa mateka kama njia ya kujipatia kipato.

Tangu kuanzishwa miaka miwili iliyopita mfumo huo uliounganishwa na ramani maalum ya kuitikia malalamiko ya jamii hasa utekaji umepokea simu 6300.