Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola milioni 75 zahitajika kusaidia wakimbizi DRC

Wakimbizi wa ndani DRC. Picha: IOM

Dola milioni 75 zahitajika kusaidia wakimbizi DRC

Shirika uhamiaji la Umoja wa Mataifa IOM limeomba dola milioni 75 kwa ajili ya kusaidia watu wanaokimbia makazi yao sababu ya machafuko nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo DRC.

Tamko hilo linafuatia ziara ya mkurugenzi wa uendeshaji na dharura wa IOM Mohamed Abdiker nchini DRC ambako amesema uwepo wa machafuko maeneo mengi duniani umelifanya eneo hilo kusahaulika ilihali kuna uhitaji mkubwa wa misaada ya kibinadamu kwa wakazi wa eneo hilo pamoja na wale wanaowasaidia.

Abdiker ameyataja maeneo yenye machafuko kuwa ni majimbo ya Kivu Kusini, Tanganyika na Kasai ambayo  yamesababisha watu zaidi ya milioni 2.5 kuyakimbia makazi yao huku machafuko yakiendelea kutokea kila uchao Kivu Kaskazini.

DRC ni nchi inayoongoza barani afrika kwa kuwa na idadi kubwa ya watu waliokimbia makazi yao kutokana na misuguano baina ya jamii hali inayosababisha zaidi ya watu milioni 4.1 kusalia wakimbizi wa ndani au nje ya nchi  yao.