Al-Shabaab wasababisha majeruhi wengi Somalia: UM

11 Disemba 2017

Mzozo nchini Somalia unaendelea kusababisha maafa makubwa dhidi ya raia, ukiharibu miundombinu na vyanzo vya mapato, kulazimisha maelfu kukimbia makwao na kukwamisha upelekaji misaada ya kibinadamu kwa wanayoihitaji, imesema ripoti ya Umoja wa Mataifa ilichapishwa Jumapili.

Ripoti hiyo itwayo “Ulinzi wa Raia: Kujenga Msingi wa Amani, Usalama na Haki za Binadamu nchini Somalia,” ambayo imechapishwa na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Usaidizi nchini Somalia (UNSOM), inaangazia matokeo yalioshuhudiwa kwanzia Januari Mosi 2016 hadi Octoba 14, 2017.

Katika kipindi hicho, UNSOM ilisajili jumla ya raia 2,078 waliouauwa na wengine 2,507 waliojeruhiwa.

Zaidi ya asilimia 60 ya majeruhi yalihusishwa na wanamgambo wa Al-shabab, asilimia 13 kwa wanamgambo wa kikoo, asilimia 11 walihusishwa na vyombo vya dola vikiwemo polisi na jeshi, huku, asilimia 4 ya majeruhi hao wakihusishwa walinda amani wa Muungano wa Afrika, AMISOM, na asilimia 12 kwa washambuliaji wasiofahamika.

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Somalia ambaye pia ni Mkuu wa Ujumbe wa Misaada wa Umoja huo, UNSOM, Michael Keating, amesema raia wamekuwa wahanga wakuu wa kushindikana kwa upatikanaji wa suluhu la kisiasa kwa mizozo nchini Somalia.

Amesema kinachoaibisha ni kwamba pande zinazozozana zinazembea kuwapa ulinzi raia wakati wa makabiliano

Ripoti hiyo imezitaka pande zinazozozana kufanya kila wawezalo kulinda raia na mali zao.

Wakati huohuo walinda AMISOMA wametakiwa kuimarisha mbinu za kuwawajibisha wanaohusika na mashambulizi dhidi ya raia.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter