Kilio cha Tanzania na Uganda kwa usaidizi chasikika- CERF
Umoja wa Mataifa umetangaza mgao wa dola milioni 100 kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya dharura ya kibinadamu kwenye nchi tisa duniani ambako operesheni za usaidizi zimekumbwa na ukata.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametangaza hayo mjini New York, Marekani wakati wa kikao cha mwaka cha kuchangisha fedha kwa ajili ya mfumo wa dharura CERF.
Ametaja nchi hizo kuwa ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Uganda, Tanzania, Cameroon, Mali, Ufilipino, Eritrea, Haiti na Pakistan, ambapo baadhi yao zinahifadhi wakimbizi na nyingine zina wakimbizi wa ndani kutokana na majanga ya asili na mapigano.
(Sauti ya Antonio Guterres)
“Fedha hizi kutoka CERF zitawezesha mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau wake kutekeleza operesheni muhimu za kuokoa maisha na kuchangia katika mnepo na utulivu wa muda mrefu.”
Bwana Guterres ametumia kikao hicho kuelezea vile ambavyo mwelekeo unavyoonyesha kuwa mizozo itaendelea huku fungu la CERF likiwa lina pengo la dola bilioni 11.
(Sauti ya Antonio Guterres)
“Ni muhimu kusaidia maisha ya shughuli za kujikimu kwa mamilioni ya watu wakiwemo wanawake, wasichana, wanaume na wavulana ambao wanategemea misaada ya kibinadamu ili kujikwamua kutoka kwenye majanga na kuwapatia matumainiya siku zijazo.”