Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mjadala wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa waanza leo

Mjadala wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa waanza leo

Hii leo mjadala wa ngazi ya juu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaanza ukitoa fursa kwa viongozi wa nchi wanachama kutoa hotuba zao kuhusu hoja mbali mbali ikiwemo masuala ya amani, usalama na maendeleo.

Kwa mujibu wa ratiba, mkutano  huo utaanza kwa hotuba ya Katibu Mkuu wa Umoja huo Ban Ki-moon akifuatiwa na hotuba ya ufunguzi kutoka kwa Rais wa mkutano wa 71 wa Baraza Kuu Peter Thomson.

Mara baada ya hotuba hiyo ya ufunguzi, viongozi wa nchi 193 wanachama wa Umoja huo wataanza kutoa hotuba zao zitakazorushwa moja kwa moja kupitia televisheni ya mtandaoni ya Umoja wa Mataifa, Webtv.un.org.

Kama ilivyo ada hotuba ya kwanza ya viongozi itatoka kwa Rais wa Brazil Michel Temer akifuatiwa na Rais Barack Obama wa Marekani.

Chad itakuwa ni ya tatu ikifuatiwa na Ufaransa ambapo kwa mujibu wa ratiba hiyo, Rais Yoweri Museveni wa Uganda anatarajiwa kuhutubia nyakati za mchana pamoja an Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini.

Utaratibu, ni kwamba marais na wakuu wa nchi ndio hupatiwa fursa za siku za mwanzoni kuhutubia wakifuatiwa na makamu Rais, mawaziri wakuu na hatimaye mawaziri wanaowakilisha nchi zao.

Mjadala huo wa wazi wa ngazi ya juu utaendelea hadi tarehe 26 mwezi huu wa Septemba.

Kando mwa mjadala huo wa wazi, kutafanyika vikao vya kando kama vile kudhibiti usugu wa dawa za kuua wadudu mashambani, utiaji saini mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, halikadhalika kikao kuhusu upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama.