Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kikao cha 71 cha baraza Kuu kimefunga pazia:

Kikao cha 71 cha baraza Kuu kimefunga pazia:

Kikao cha 71 cha baraza kuu la Umoja wa Mataiofa leo kimefunga pazia kwenye makao makuu ya Umoja huo hapa New york Marekani. Akizungumza katika mkutano wa ufungaji wa kikao hicho Katibu Mkuu wau moja wa Mataifa Antonio Guterres amemshukuru Rais wa kikao cha 71 Peter Thompson kwa kazi nzuri aliyoifanya kwa mwaka mzima

(GUTERRES CUT 1)

“Asante kwa maono yako, asante kwa ushupavu wako, asante kwa sauti yako isiyokosea ambayo imetukumbusha baadhi yetu misingi ya shule ya grama, lakini zaidi ya yote asante kwa kusaidia kuziweka nchi wanachama katika rekodi imara ya mafanikio kwa mwaka uliopita . Usiku na mchana, ulituleta pamoja.

image
Katibu Mkuu Antonio Guterres akizungumza kwenye ufungaji wa kikao cha 71 cha baraza kuu. Picha na UM
Ameongeza kuwa kikao cha 71 kimeshuhudia mafanikio makubwa ikiwepo mkutano wa kimataifa wa wakimbizi na wahamiaji na kupitishwa azimio la kihistoria kushughulikia changamoto zinazowakabili watu hao. Pia amesema hatua muhimu zilizochukuliwa kuchagiza ajenda ya 2030 ya maendeleo endelevu au SDG’s ikiwemo kuanzishwa bank ya teknolojia kwa ajili ya nchi zenye maendeleo duni na mkutano wa masuala ya baharí mwezi juni mwaka huu ulidhihirisha changamoto zinazoyakabili mataifa ya visiwa vidogo vinavyoendelea na kusisitiza kuwa kwa mwaka uliopita baraza kuu

(GUTERRES CUT 2)

“limeendelea kutumika kama jukwaa la kushinikiza masuala ya kimataifa kuanzia usafirishaji haramu wa binadamu hadi usugu wa vijiuadudu vinavyoleta maradhi.nimeridhika kuona milango ya baraza kuu inagfunguka hata zaidi kwa wadau muhimu kama asasi za kiraia, sekta binafsi na zaidi ya yote kwa vijana,.”

Ameongeza kuwa kikao cha 71 pia kilikuwa na jukumu la kuchagua Katibu Mkuu mpya wa Umoja wa Mataifa amekipongeza kwa utaratibu mzuri uliotumika na wa wazi. Na kwa Rais mpya wa kikao cha 72, Miroslav Lajcak, amemwambia umoja wa Mataifa unatarajia kushirikiana naye na kuhakikisha kikao cha 72 kinakuwa cha mafanikio kwa kuhudumia watu wa dunia.

image
Rais wa kikao cha 71 cha baraza kuu la Umoja wa Mataifa Peter Thompson. Picha na UM
Naye Peter Thompson Rais wa kikao cha 71 ambaye kipaumbele chake kilikuwa utekelezaji wa SDG’s akiaga kwenye mkutano huo amewashukuru viongozi mbalimbali kwenye Umoja wa Mataifa akiwemo Katibu mkuu , nchi wanachama na kutaja masuala mbalimbali yaliyofanikiwa katika muhula wake hana kusisitiza masuala saba muhimu

(PETER THOMPSON CUT)

“Moja naamini kwa pamoja tumefanikiwa kuchagiza mchakato wa SDG’s, pili kuna hatua za kimataifa zilizopigwa katika masuala muhimu, lakini hatua za SDG’s mashinani haziwiani kikanda, kijinsia na miongoni mwa rika , na hata baina ya mijini na vijijini , tatu pengo la ufahamu kuhusu SDG’s duniani bado ni kubwa ambalo ni lazima tulirekebishe, nne kuna pengo pia kwenye mfumo wa Umoja wa Mataifa katika kusaidia nchi kutekeleza malengo ya maendeleo.”

Tano amesema mkutano wa masuala ya bahari ulidhihirisha uwezo wa kuwaleta wadau wote katika kutatua changamoto za dunia za utekelezaji wa SDG’s, sita amesema kunahitajika mabadiliko katika suala la ufadhili na mwisho amechagiza nchi wanachama na jumuiya ya kimataifa kukumbatia uwezo wa teknolojia na ubunifu katika utekelezaji wa SDG’s. Kikao cha 72 cha baraza kuu kitaanza rasmi Kesho Jumanne.