Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Boko Haramu yazidi kuwafungisha watu virago Mashariki mwa Niger:UNICEF

Boko Haramu yazidi kuwafungisha watu virago Mashariki mwa Niger:UNICEF

Ghasia zinazohusishwa na kundi lenye itikadi kali la Boko Haramu Mashariki mwa Niger zimesababisha wimbi kubwa la watu kufungasha virago , limeonya leo Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto(UNICEF).

Takribani watu 67,000 inaaminika wamekimbia makwao kutokana na mashambulizi tangu mwanzo wa mwezi huu , na sasa ongeza wengine 240,000 ambao tayari walishatawanywa na machafuko kwenye mkoa wa Diffa.

Kwa mujibu wa UNICEF wanaosaka malazi wengi wao ni wakimbizi wa kiNigeria na wakimbizi wa ndani kutoka Nigeria ambao wameweka maskani kando ya barabara kuu ijulikanayo kama Route Nationale 01.

Kutoka Niger huyu hapa Viviane van Steirteghem,wa UNICEF...

(SAUTI YA VIVIANE)

"Hili limeongeza shinikizo kubwa katika rasilimali hususani maji, kwa sababu watu wapya wanaowasili katika maeneo makubwa matatu , hawajafika kukaa na familia zao tu bali pia wamekuja na ng’ombe zao”

Wengi wa watu wapya wanaowasili ni wanawake na watoto, kana inavyosema UNICEF , wanaume wamesalia nyumbani karibu na ziwa Chad ili kupanda mazao kwa kuwa msimu wa mvua umeanza”.