Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bi. Catherine Samba-Panza, kiongozi mpya wa mpito CAR: BINUCA yapongeza

Bi. Catherine Samba-Panza, kiongozi mpya wa mpito CAR: BINUCA yapongeza

Baraza la Taifa la mpito huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR limemchagua Meya wa mji mkuu Bangui, Bi. Catherine Samba-Panza kuwa Mkuu mpya wa mamlaka ya mpito nchini humo.

Hatua hiyo imepatiwa pongezi na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya ujenzi wa amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, BINUCA ambayo imesifu kasi iliyoonyeshwa na wanachama wa baraza la mpito kufanikisha suala hilo.

Taarifa ya BINUCA imesema uchaguzi wa Bi. Samba-Panza umeashiria mwanzo mpya wa nchi hiyo kusonga mbele katika kurejesha demokrasia ikiwemo kufanya mashauriano ya demokrasia yaliyo huru na ya wazi.

Wakati kiongozi huyo mpya wa mpito akijiandaa kuteua Waziri Mkuu pamoja na serikali, BINUCA imetaka viognozi wa kisiasa kusonga mbele na kushiriki kumaliza ghasia zinazoendelea kuweka mgawanyiko mkubwa miongoni mwa jamii nchini humo.

BINUCA imesema wakati ni huu na pande zote na jumuiya ya kimataifa inapaswa kuutumia vyema ili kuanza ukurasa mpya.

Uteuzi wa Bi. Samba-Panza umekuja baada ya kujiuzulu kwa viongozi wa awali mapema mwezi huu  huu.