Rais wa baraza kuu la UM kuzuru Ethiopia wiki hii

2 Machi 2016

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Mogens Lykketoft atazuru Ethiopia kuanzia Alhamisi Machi 3 hadi Ijumaa Machi 4 kukutana na viongozi wa serikali, viongozi wa Umoja wa Mataifa, kuhutubia Muungano wa Afrika na kukutana na wakimbizi.

Baada ya kuwasili Addis Ababa Alhamisi, bwana Lykketoft atasafiri na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR hadi kwenye kambi kukutana na wakimbizi waliokimbia machafuko Sudan Kusini.

Siku ya Ijumaa atakutana na mwenyekiti wa tume ya Muungano wa Afrika Dr. Nkosazana Dlamini-Zuma kabla ya kuhutubia kamati ya wawakilishi wa kudumu wa tume ya Muungano wa Afrika.

Baadaye siku hiyo atakutana pia na Rais wa Ethiopia Dr. Hailemariam Desalegn, Waziri Mkuu na Bwana Haile Menkerios, ambaye ni mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa kwenye Muungano wa Afrika (AU).

Bwana Lykettoft atazungumzia umuhimu wa ushirikiano baina ya Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika kwenye warsha ya jumuiya za kiraia kabla ya kurejea New York siku ya Jumamosi.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter