Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miaka 65 tangu tamko la haki za binadamu, bado haki zinabinywa: Eliasson

Miaka 65 tangu tamko la haki za binadamu, bado haki zinabinywa: Eliasson

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na kikao maalum kuhusu haki za binadamu kikiangazia mustakhbali wa sualahiloikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya kimataifa ya haki za  binadamu.

Wakati wa kikao hicho Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan Eliasson alieleza bayana kuwa miaka 65 tangu kupitishwa kwa tamko la kimataifa la haki za binadamu, kuna mafanikio yamepatikana ikiwemo kuanzishwa kwa vyombo vya kitaifa na kimataifa vya kusimamia haki.

Hata hivyo amesema bado kuna changamoto kwani bado haki hizo zinabinywa ilhali tamkohilolilitaka kila mtu kupata haki za msingi bila kujali rangi yake, imani yake ya kidini au hata uwezo wake wa kiuchumi na kijamii.

(Sauti ya Jan Eliasson)

“Ni jukumu la kila nchi mwanachama kwanza kulinda haki za binadamu na kuepusha ukiukwaji wa haki katika ngazi ya kitaifa. Halafu ni jukumu la nchi wanachama kwa ujumla kuchukua hatua stahiki pindi kitendo cha nchi nyingine  kushindwa kusimamisha haki za binadamu kinaposababisha janga kubwa na mauaji. Tunapaswa kuongeza jitihada zaidi angalau kupitia tathimi za kipindi kuhakikisha nchi zinatimiza wajibu wao.”

Siku hiyo imeenda sanjari na kutoa tuzo kwa washindi Sita wa tuzo ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa kwa mwaka huu wa 2013.