Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban aunda kamisheni ya ajira sekta ya afya, kuongozwa na Zuma na Hollande

Ban aunda kamisheni ya ajira sekta ya afya, kuongozwa na Zuma na Hollande

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameunda kamisheni kuhusu ajira katika sekta ya afya na ustawi wa uchumi itakayoongozwa na Marais Jacob Zuma wa Afrika Kusini na Francois Hollande wa Ufaransa.

Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa imesema kamisheni hiyo imeanzishwa kwa kuzingatia kuwa ukuaji wa uchumi duniani unatarajiwa kuanzisha zaidi ya fursa Milioni 40 za ajira kwenye sekta ya afya ifikapo mwaka 2030.

Hata hivyo Ban amesema katika nchi za kipato cha chini na cha kati bado kuna pengo la wahudumu katika sekta hiyo ya afya, wakati ni muhimu wawepo wa kutosha kila nchi duniani ili kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu.

Kwa mantiki hiyo kamisheni hiyo ambayo makamishna wake 25 watateuliwa baadaye, itakuwa na jukumu la kupendekeza hatua za kuchukua kuondoa pengo hilo na kuweka fursa za ajira kwenye sekta hiyo ili kuhakikisha ukuaji uchumi jumuishi.

Kamisheni hiyo imeundwa kwa kuzingatia azimio namba A/RES/183 ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa linalotambua umuhimu wa kuwekeza katika nguvukazi mpya kwenye sekta ya afya ili kfuanikisha ajenda 2030.

Mkutano wa kwanza wa kamisheni hiyo utafanyika tarehe 23 mwezi huu na ripoti yake kutarajiwa kando mwa mkutano wa 71 wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Septemba mwaka huu.