Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Takwimu pekee hazitoshi kuunda sera dhidi ya umaskini: Benki ya Dunia

Takwimu pekee hazitoshi kuunda sera dhidi ya umaskini: Benki ya Dunia

Kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani leo kumekuwa na mjadala maalum ulioandaliwa na Benki ya Dunia kuhusu kiwango cha umaskini.

Katika hotuba yake, Kaushik Basu, mchumi mkuu kwenye Benki ya Dunia amesema cha msingi katika kutokomeza umaskini ni kuhakikishia tofauti za kiuchumi zinapungua na ukuaji wa uchumi unawanufaisha hata watu maskini.

Amemulika umuhimu wa takwimu akieleza kwamba Benki ya Dunia hivi karibuni imebadilisha kiwango cha umaskini duniani kwa kukiongeza kutoka dola 1.25 kwa siku hadi kufikia dola 1.9 ili kwenda sambamba na ongezeko la bei za bidhaa duniani.

Mathalani mwaka 1990, asilimia 40 ya watu duniani kote walikuwa wakiishi na kipato cha chini ya kiwango cha umaskini wakati ambapo idadi hiyo imefika asilimia 13 mwaka 2012, lakini barani Afrika bado idadi hiyo ni asilimia 46.

Hata hivyo Bwana Basu amesisitiza umuhimu wa kutotegemea takwimu tu katika uundaji wa sera na mikakati.

(Sauti ya Bwana Basu)

“ Ni kitu ambacho nasisitizia sana, kwamba siku hizi tuna ujuzi zaidi kuhusu ukusanyaji takwimu, lakini kutoka takwimu hadi sera, ni lazima kufanya uchambuzi. Hatupaswi kupuuza uchambuzi, ikiwa tunataka kupata sera bora kuhusu usaidizi wa chakula au afya kwa mfano, unahitaji kufanya uchambuzi bora wa takwimu ulizonazo na kuzungumzia harakati za kisera.”