Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashirika ya UM yajiandaa kwa kimbunga Yemen

Mashirika ya UM yajiandaa kwa kimbunga Yemen

Ofisi ya kuratibu masuala ya kibinadamu, OCHA, imesema kuwa mashrika ya Umoja wa Mataifa yanajiandaa kutoa misaada nchini Yemen, wakati kimbunga cha daraja ya tatu kiitwacho Chapala kikitarajiwa kufika nchi kavu saa tatu asubuhi Jumanne mnamo Novemba tatu.

Kwa mujibu wa OCHA, kimbunga hicho kinaikaribia Yemen kutokea upande wa kusini.

OCHA imesema kuwa madhara ya kimbunga Chapala huenda yakaathiri maeneo mengi ya Yemen, lakini yaweza yakawa mabaya zaidi katika mikoa ya Shabwah na Hadhramaut. Mikoa hiyo kwa pamoja ina idadi ya watu milioni 1.8, ambao milioni 1.4 katia yao tayari wanahitaji usaidizi wa kibinadamu, kulingana na tathmini ya mahitaji ya kibinadamu iliyofanywa na Umoja wa Mataifa.

Idadi ya watu wanaohitaji usaidizi inajumuisha wakimbizi wa ndani 100,000 na zaidi ya wakimbizi na wahamiaji 27,000.

Tayari kisiwa cha Yemen cha Socotra kimeshaathiriwa na kimbunga hicho mnamo Novemba mosi, ambako kimeharibu nyumba zipatazo 20 na kulazimu zaidi ya watu 1,200 kuhamishwa kwa dharura.