Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkataba dhidi ya rushwa waangaziwa, azimio la kudhibiti latarajiwa:

Mkataba dhidi ya rushwa waangaziwa, azimio la kudhibiti latarajiwa:

Mkutano wa Sita wa nchi wanachama wa mkataba wa kimataifa dhidi ya rushwa, umeanza leo huko St. Petersburg nchini Urusi ambapo mwishoni mwa mkutano wajumbe wataridhia azimio la kuimarisha vita dhidi ya rushwa. Joshua Mmali na ripoti kamili.

(Taarifa ya Joshua)

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon kwenye ujumbe wake kwa washiriki wa mkutano amekumbusha kuwa rushwa na ufisadi lazima vikome ili kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kudhibiti madawa ya kulevya na uhalifu, UNODC, Yury Fedotov akihutubia wajumbe amesema kikao kinafanyika wakati muafaka ambapo tayari dunia imeridhia malengo hayo, akitaja namba 16 linalozingatia suala la utoaji haki.

Amesema rushwa ni kikwazo cha haki na iwapo haitapatiwa kipaumbele itakwamisha ufanikishaji wa malengo hayo endelevu kwa ustawi bora wa wakazi wa ulimwenguni.

Kwa mantiki hiyo amesema ni matumaini yake washiriki wataridhi rasimu ya azimio ambayo pamoja na mambo mengine inaleng kushughulikia changamoto kadhaa ikiwemo ubia kati ya sekta binafsi na umma kwenye kudhibiti rushwa, kupokonya mali zilizopatikana kwa misingi ya rushwa na matumizi ya sayansi ya teknolojia.

Kenya, Tanzania na Uganda ni miongoni mwa nchi 177 zilizotia saini na kuridhia mkataba huow a kudhibiti rushwa duniani.