Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Upatikanaji wa ARV’s kwa wenye VVU kutaepusha vifo Milioni 21:WHO

Upatikanaji wa ARV’s kwa wenye VVU kutaepusha vifo Milioni 21:WHO

Shirika la Afya Duniani, WHO limesema mtu yeyote aliyeambukizwa virusi vya Ukimwi anapaswa kuanza tiba ya kupunguza makali ya ugonjwa huo, yaani Anti-Retroviral Therapy, ART haraka iwezekanavyo baada ya uchunguzi.

Kwa mujibu wa WHO pendekezo hilo la “Tibu Kila Mtu” limeondoa uzuizi wa awali wa matumizi ya ART miongoni mwa watu wanaoishi na ugonjwa huo, na kwa maantiki hiyo, watu wote sasa bila kujali umri wao wanafaa kupata matibabu hayo.

Kupanuliwa kwa matumizi ya tiba ya ART kunaungwa mkono na matokeo ya hivi karibuni kufuatia majaribio ya kliniki yaliyothibitisha kuwa matibabu ya mapema yanawasaidia watu wenye VVU kuishi muda mrefu zaidi wakiwa na afya bora huku wakipunguza hatari ya kuwaambukiza wenzao kirusi hicho.

Kulingana na makadirio ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshuighulika na masuala ya ukimwi UNAIDS kupanuliwa kwa matumizi ya ART’s kwa watu wote wanaoishi na Ukimwi sawa na kupanuliwa kwa uchaguzi wa kuzuia kunaweza kusaidia kuepusha vifo vya watu milioni 21 wanayohusiana na maambukizi milioni 28 mapya ifikapo mwaka 2030.