Kwa umoja ule ule kwenye SDGs, tushirikiane pia kuondoa silaha za nyuklia:Ban
IKwa umoja ule ule kwenye SDGs, tushirikiane pia kuondoa silaha za nyuklia:Ban
Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya kutokomeza matumizi ya silaha za nyuklia, Baraza kuu la Umoja wa Mataifa limeitisha mkutano usio rasmi kuhusu suala hilo ikiwa ni miaka 70 tangu silaha ya nyuklia kutumika dhidi ya binadamu huko Nagasaki na Hiroshima.
Akizungumza kwenye mkutano huo uliohusisha pia Iran katika maandalizi, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema umefanyika wakati muafaka ambapo dunia inaahidi kuwa kamwe hakuna binadamu mwingine atakumbwa na kisanga cha madhara ya silaha za nyuklia.
Ban amesema kwa miongo saba, azma ya kutokuwa na silaha za nyuklia imekuwa thabiti lakini dunia itakuwa salama iwapo zitaondolewa kabisa duniani.
Amesema viongozi wa dunia kupitia malengo ya maendeleo endelevu wameahidi kulinda dunia kwa kutambua kuwa binadamu wote wanatumia sayari moja kwa pamoja na hivyo kwa misingi hiyo hiyo walinde sayari dhidi ya silaha za nyuklia ambazo zinatishia uwepo wa wakazi wote wa dunia.
Hivyo Katibu Mkuu ametoa wito kwa wakazi wa dunia kusimama kidete na kutaka kuchukuliwa kwa hatua akisema matumaini yake ni kwa vijana ambao mara nyingi viongozi wanaamini hawana uwezo wa kujenga amani lakini yeye binafsi anaamini ndio wakati wao na wanao uwezo wa kufanya hivyo.