Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Huduma za afya zaimarika Tanzania: Kikwete ashiriki uzinduzi wa mradi wa kimataifa

Huduma za afya zaimarika Tanzania: Kikwete ashiriki uzinduzi wa mradi wa kimataifa

Shirika la Afya Duniani WHO, Benki ya Dunia pamoja na Mfuko wa Bill na Melinda Gates wamezindua mradi mpya wa ubia kwa ajili ya kuimarisha upatikanaji wa huduma za msingi za afya kwenye nchi zenye kipato cha chini na cha kati.

Mradi wa ufanisi wa huduma za msingi za afya, PHCPI umezinduliwa leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa wakati ambapo viongozi wa kimataifa wameridhia malengo ya maendeleo endelevu, ambapo lengo namba Tatu kuhusu afya linataka huduma za afya kufikia watu wote ifikapo mwaka 2030.

Mradi huo unatarajia kuimarisha upatikanaji wa takwimu kuhusu huduma za afya, pia ushirikiano baina ya nchi.

Akiongea wakati wa uzinduzi huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema mlipuko wa Ebola mwaka jana umeonyesha umuhimu wa kutegemea huduma za msingi za afya imara.

“Tunajua kwamba milipuko mipya ya ugonjwa isiyotarajiwa itatokea kwenye miaka ijayo. Hii ni lazima. Hatujui tu ni lini, wapi na vipi itatokea. Jamii ambazo zinakabili mapema na changamoto hizo, na kushiriki huduma zao za afya, ni msingi wa nchi na dunia yenye usalama zaidi.”

Kwa upande wake Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete ameeleza mafanikio yaliyopatikana katika kueneza huduma za afya za msingi nchini Tanzania.

(Sauti ya Rais Kikwete)

Kwa mujibu wa WHO bado watu milioni 400 duniani kote wanakosa huduma za msingi za afya.