Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

OECD na UNCTAD washirikiana kufanikisha Ajenda ya Maendeleo Endelevu

OECD na UNCTAD washirikiana kufanikisha Ajenda ya Maendeleo Endelevu

Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo, OECD na Kamati ya Biashara na Maendeleo ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD yameahidi kufanya kazi kwa pamoja katika maeneo ya umuhimu kwa Ajenda ya Maendeleo Endelevu yaliyopitishwa Ijumaa na vongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.

Katibu Mkuu wa OECD, Jose Ángel Gurría na Katibu mkuu wa UNCTAD Mukhisa Kituyi walisaini makubaliano ya ushirikiano wakati wakihudhuria mkutano wa 70 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Katika taarifa ya pamoja viongozi hao wa UNCTAD na OECD wamesema wanaamini biashara na uwekezaji ni muhimu kwa maendeleo na kuafikia malengo mapya yaliyokubaliwa kwa minajili ya kukuza ustawi wa pamoja na kwa wote katika kipindi cha miaka 15 zijazo.

Halikadhalika mashirika hayo yamesema yatafanya kazi kwa pamoja ili kujenga mazingira mazuri ya ukuaji wa uchumi, ajira bora sawa na kuboresha uendelevu wa kitaifa na kimataifa wakati wa kuelekea uchumi wa kimataifa uliojikita katika kanuni na maadili duniani kwa manufaa ya nchi zote na kupunguza umaskini duniani.