Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ajenda ya Maendeleo Endelevu 2030 itaendeleza gurudumu la MDGs- Bi Mohammed

Ajenda ya Maendeleo Endelevu 2030 itaendeleza gurudumu la MDGs- Bi Mohammed

Mshauri maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs, Amina Mohammed, amesema kuwa wakati Umoja wa Mataifa ukiadhimisha miaka 70 tangu kuanzishwa kwake, ni vyema kuwa umoja huo umeweka nguzo muhimu ya maendeleo, kwa kuunda ajenda ya maendeleo endelevu ya 2030, ambayo malengo yake 17 yatapitishwa mwishoni mwa wiki hii.

Bi Mohammed amesema ingawa kuna changamoto nyingi duniani, ikiwemo mizozo, wengi wakihoji iwapo ajenda hiyo itatosha kushughulikia changamoto hizo, kuafikia ajenda hiyo tayari ni hatua kubwa ya ufanisi. Aidha, amesema ajenda hiyo haitaacha malengo ya maendeleo ya milenia ambayo hayakutimizwa nyuma, bali itayapa msukumo.

Bi Mohamed ameeleza kilicho tofauti sasa, ukilinganisha malengo ya maendeleo endelevu na malengo ya maendeleo ya milenia, yanayofikia ukomo wake mwaka huu..

“Nadhani hatua tuliyoenda zaidi kutoka kwa MDGs, ni kwamba tumeshughulikia suala la ufadhili na jinsi ya kutekeleza kabla ya kuafikia malengo. Huo ulikuwa ufanisi kweli Addis. Ilikuwa kazi ngumu, kuna vitu ambavyo havikumfurahisha kila mtu, lakini tulichopata na mkakati unaoenda mbali zaidi, kuangalia rasilmali za kitaifa na masuala ya utawala, na kuweka jukwaa la teknolojia, ambayo ni muhimu kwa wakati huu, na kufungua matrilioni ya fedha tunazohitaji kwa haya, ambazo ni dhahiri kuwa zipo.”

Bi Mohammed amesema ajenda hiyo ni yenye maana na jumuishi, ikiwakilisha kila mtu.

“Ni ajenda ya wote, kwa hiyo inamgusa kila mtu. Hatutakuwa tena na kauli za kaskazini na kusini, kuhusu nini kaskazini inafanyia kusini, lakini ni nini tunachofanyiana kwa ajili yake.”