Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban ahimiza nchi ziongeze juhudi kukabiliana na usafirishaji haramu wa watu

Ban ahimiza nchi ziongeze juhudi kukabiliana na usafirishaji haramu wa watu

Ikiwa leo ni siku ya kupinga usafirishaji haramu wa watu, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, amesema uhalifu huo hunawiri katika nchi ambako utawala wa sheria ni hafifu na ushirikiano wa kimataifa ni mgumu. Taarifa kamili na Amina Hassan.

(Taarifa ya Amina)

Bwana Ban ametoa wito kwa nchi zote zikabiliane na ulanguzi wa fedha na kusaini na kuridhia mikataba ya Umoja wa Mataifa dhidi ya ufisadi na uhalifu wa kupangwa kimataifa, ukiwemo ule unaohusu usafirishaji haramu wa watu.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na dawa za kulevya na uhalifu, Yury Fedotov, amesema mamilioni ya watu wananyanyaswa, wakilazimishwa kufanya kazi viwandani, mashambani, katika biashara ya ngono, kuombaomba mitaani, kutumikishwa vitani, ndoa za lazima, na wengine kunyofuliwa viungo vyao vya mwili ili viuzwe.

"Wanawake, wanaume na watoto wanaosafirishwa kiharamu ni waathirika wa uhalifu, iwe wanatumikishwa ndani ya nchi yao au nje ya mipaka. Hatuna budi ila kuwapa matumaini na haki zao, na wahalifu wanaopanga usafirishaji huo haramu ni lazima waadhibiwe, na waathirika wapewe huduma wanayostahili."

Bwana Fedotov amesema hatua ya kwanza ya kukabiliana na usafirishaji haramu wa watu ni kulitilia zaidi maanani tatizo hilo