Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mifuko ya kukimu na kunusuru jamii bado yahitajika nchi zinazoendelea: Ripoti

Mifuko ya kukimu na kunusuru jamii bado yahitajika nchi zinazoendelea: Ripoti

Idadi kubwa ya nchi zinazoendelea zinawekeza katika mifuko ya kukimu jamii kwa lengo la kukwamua maisha ya mabilioni ya watu maskini na wale walioko hatarini zaidi, imesema ripoti mpya ya Benki ya dunia kuhusu hali ya mipango ya kunusuru kaya na kujikimu iliyotolewa leo.

Ripoti hiyo hata hivyo inasema bado watu zaidi ya milioni 770 ambao ni sawa na asilimia 55 ya watu maskini zaidi duniani hawana fursa ya kupata huduma hiyo adhimu, hasa kwenye nchi za vipato vya chini na mijini.

Kwa mantiki hiyo ripoti hiyo inataka mkutano wa ufadhili kwa maendeleo utakaoanza Addis Ababa Ethiopia wiki ijayo uweke mikakatiya kuhakikisha serikali zinaanzisha au zinatunisha mifuko hiyo ili iwafikie walengwa wengi zaidi.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo hadi sasa zaidi ya watu Bilioni Moja nukta Tisa katika nchi 136 za vipato vya chini na kati ni wanufaika wa mipango ya kijamii ya kujikimu ambapo benki ya dunia kupitia mkurugenzi mwandamizi wa masuala ya hifadhi ya jamii Arup Banerji inasema ni ushahidi tosha kuwa mpango huo umebadili maisha ya kaya hizo.

Mpango wa kusaidia kaya maskini kujikimu huhusisha shughuli mbali mbali ikiwemo kushiriki katika kazi za umma na kupatiwa ujira ambapo huweza kugharimia huduma mbali mbali kama vile elimu na afya.